Shina la wakereketwa Mlandege imani kwa CCM – Kihongosi

IRINGA: Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi amezindua Shina la Wakereketwa lililopo Stendi ya Mlandege, Kata ya Kwa Kilosa mkoani Iringa.
Kihongozi amezindua shina hilo leo Juni 20,2026 huku akiwapongeza wanachama wa eneo hilo kwa kujitolea kujenga shina hilo, akisema wameonesha kwa vitendo mapenzi yao kwa CCM.

Akizungumza mara baada ya kuzindua shina hilo, Kihongosi alisema ujenzi wa shina hilo pamoja na ushiriki mkubwa wa wanachama ni ushahidi wa imani na mshikamano mkubwa waliounao kwa CCM.
“Kwanza tuwapongeze sana wanachama wote wa tawi hili na shina hili kwa kujenga shina zuri ambalo lina ubora mzuri ambao tunauona hapa. Tunapigia makofi mama yetu Mama Seki kwa kazi hii nzuri na kubwa ambayo ameifanya,” alisema.

Alisema wanachama wa tawi hilo wameonesha wazi kuwa wana mapenzi makubwa kwa CCM na wanaendelea kukiamini chama hicho kuwa ndicho chombo muhimu cha kuwaletea maendeleo wananchi wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.

“Lakini tuwapongeze wanachama mia moja katika tawi hili na shina hili. Wamedhihirisha kwa dhati kwamba wana mapenzi makubwa na CCM na bado tunaamini kwamba Chama Cha Mapinduzi ndiyo chama pekee ambacho kitaleta maendeleo katika mkoa wetu wa Iringa na taifa letu kwa ujumla,” amesema Kihongosi.
Kihongosi aliwataka wanachama kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa na Serikali pamoja na chama katika maeneo yao.



