Sherehe za Kiswahili zafana Algeria

BALOZI wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, amesema lugha ya Kiswahili inaendelea kukua duniani, ikiwa sasa inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 katika nchi 14 na kutumika rasmi katika jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa.

Balozi Matinyi amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria na kufanyika jijini Algiers Julai 9, mwaka huu.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, taasisi za umma na binafsi, wanazuoni na waandishi wa habari, zikiongozwa na Katibu Mnadhimu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Algeria, Bibi Nacera Ayaïchia.

Akizungumzia kuhusu Kiswahili, huku hotuba yake ikitafsiriwa kwa Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza, Balozi Matinyi alisema Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Tanzania na pia kinatumika kama lugha ya taifa katika Kenya, Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Aidha amesema Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Ameongezea kuwa redio mbalimbali za kimataifa zikiwemo za Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Japan, China, Iran na India hutangaza vipindi vya Kiswahili, jambo linalodhihirisha kuendelea kwa ukuaji wa lugha hiyo duniani.

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu, “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani,” Balozi Matinyi alisema lugha hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha mshikamano, kudumisha amani na kukuza ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.

SOMA: Kiswahili hazina ya Tanzania

Sherehe hizo zilipambwa na maonesho ya utamaduni wa Tanzania yaliyohusisha chai na kahawa ya Tanzania, vyakula vya asili vya Kiswahili, pamoja na mavazi ya pwani ikiwemo khanga, baibui, kanzu, vikoi na vitenge vilivyovaliwa na wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini Algeria.

Maadhimisho hayo yalijumuisha pia kuoneshwa kwa filamu fupi iliyoangazia viongozi mbalimbali wa Afrika wakihutubia kwa Kiswahili katika nyakati tofauti, ikiwemo hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa nchini Comoro mwaka 2025 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo.

Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani huadhimishwa kila Julai 7 tangu mwaka 2022, kufuatia uamuzi wa UNESCO wa mwaka 2021 kuitangaza siku hiyo kuwa maadhimisho rasmi ya lugha ya Kiswahili, ikiwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kupata hadhi hiyo kimataifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button