Tamasha uhuru wa DRC kufanyika Juni 30 Dar

DAR ES SALAAM: JUMUIYA ya Wakongo waishio Tanzania inatarajia kuadhimisha miaka 66 ya Uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia tamasha kubwa litakalofanyika Juni 30, 2026, katika viwanja vya Montana, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Fariara Lengose, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuenzi historia ya taifa la Congo pamoja na kuimarisha mshikamano na urafiki kati ya wananchi wa taifa hilo na Tanzania.

Lengose amesema tamasha hilo litapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa Congo na Tanzania, huku likitarajiwa kuhudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri, wakiwemo wasanii Christian Bella, Nyoshi Elsadati, pamoja na viongozi na wadau wengine.

Kwa upande wake, King Dodo amesema tasnia ya muziki nchini Tanzania imekua kwa kiwango kikubwa, akibainisha kuwa hapo awali walikuwa wakilazimika kuwaalika wasanii kutoka Congo pekee kwa ajili ya kutoa burudani.

“Zamani tulikuwa tukiwaleta wasanii kutoka Congo, lakini kwa sasa wasanii wa Tanzania wameonyesha uwezo mkubwa na wanatoa burudani ya kiwango cha juu. Tunajivunia kazi nzuri wanayoifanya,” amesema King Dodo.

Tamasha hilo linatarajiwa kukutanisha mamia ya wakazi wa Tanzania na raia wa Congo waishio nchini katika siku ya burudani, utamaduni na kuimarisha uhusiano wa kijamii kati ya mataifa hayo mawili.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button