Elimu inahitajika kudhibiti uchafuzi wa mazingira Dar

JIJI la Dar es Salaam linaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na ongezeko la taka ngumu, matumizi holela ya plastiki, uchafuzi wa hewa, pamoja na utupaji wa majitaka usiozingatia taratibu za kimazingira.

Hali hiyo imeibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa mazingira, huku takwimu zikionesha kuwa sehemu kubwa ya taka zinazozalishwa jijini bado huishia kwenye mifereji ya maji, maeneo ya wazi na baharini, hali inayoongeza hatari ya mafuriko, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa mifumo ya ikolojia.

Tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya uchafuzi unaopatikana baharini unatokana na taka ngumu, hasa plastiki, huku kati ya asilimia 10 na 12 ya uchafuzi huo ukichangiwa na taka za plastiki zinazobebwa na mito na mifereji kutoka maeneo ya mijini kuelekea Bahari ya Hindi.

Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ni kitovu kikuu cha biashara na makazi nchini umeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu na shughuli za kiuchumi hali inayokwenda sambamba na kuongezeka kwa uzalishaji wa taka kila siku. SOMA:

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki bado ni changamoto kubwa kwa jiji hilo. “Mkoa wa Dar es Salaam ni jiji la biashara, hivyo uchafuzi wa mazingira kwa mifuko ya plastiki umekuwa dhahiri kabisa, na hii inatokana na uwepo wa viwanda bubu vingi,” alisema Chalamila.

Kwa upande wake, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema linaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake kwa kufanya ukaguzi wa viwanda, masoko na maeneo mbalimbali yanayohatarisha mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, ofisa wa baraza hilo, Glory Kombe alisema taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki. “Tutaendelea kutoa elimu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha sheria na kanuni za mazingira zinatekelezwa kwa weledi na kwa wakati,” alisema.

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira pia imeeleza kuwa uhifadhi wa mazingira umepewa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Katika taarifa yake ya hivi karibuni, ofisi hiyo ilisema Tanzania inalenga kuwa miongoni mwa nchi vinara wa utunzaji wa mazingira ifikapo mwaka 2050 kupitia utekelezaji wa mikakati ya kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza matumizi ya nishati safi na kuimarisha elimu ya mazingira kwa umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Masauni, amesema usimamizi endelevu wa taka ni miongoni mwa nyenzo muhimu za kukuza uchumi na kulinda afya za wananchi. “Usimamizi endelevu wa taka utachangia kuongeza kipato, kukuza uchumi wa nchi na uhifadhi wa mazingira,” alisema. SOMA: Tabianchi Yatikisa Kilimo cha Mwani

Wadau wa mazingira wameonya kuwa endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, Dar es Salaam itaendelea kukabiliwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na kuziba kwa mifereji, kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira pamoja na athari kwa viumbe wa baharini na shughuli za kiuchumi.

Aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema kuna haja ya kuimarisha uwezo wa NEMC ili iweze kusimamia kwa ufanisi zaidi masuala ya uhifadhi wa mazingira nchini. “Tunahitaji kuimarisha taasisi za mazingira ili ziweze kusimamia kikamilifu rasilimali zetu na kukabiliana na changamoto zinazoongezeka za uchafuzi wa mazingira,” alisema.

NEMC imeweka matarajio makubwa katika kipindi kijacho, ikiwamo kuongeza ukaguzi wa viwanda na taasisi zinazochafua mazingira, kuimarisha usimamizi wa taka, kutumia teknolojia za kisasa kufuatilia maeneo yenye mrundikano wa taka, pamoja na kuongeza ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi. Baraza hilo linaamini kuwa ushiriki wa kila mwananchi katika kutunza mazingira, kuacha kutupa taka ovyo na kuzingatia sheria za mazingira ni msingi muhimu wa kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji safi, salama na lenye mazingira endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button