Mbunge Ngajilo ahoji kukwama mradi wa barabara

IRINGA: Mradi wa barabara ya mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass) unaendelea kuwa gumzo kubwa bungeni na miongoni mwa wananchi, baada ya kazi zake kusimama katika hatua muhimu ya ujenzi, hali inayozua maswali juu ya hatima ya mradi huo wa kimkakati unaotarajiwa kubadilisha uso wa mji wa Iringa.

Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ameibua hoja hiyo bungeni akieleza changamoto zinazoikumba barabara hiyo ya Igumbilo–Kihesa, yenye ambayo mpaka kukamilika kwake itagharimu zaidi ya Sh bilioni 41.

Ngajilo alisema kuwa mradi huo umekwama baada ya mkandarasi kusitisha kazi kutokana na madai ya malipo ya zaidi ya Sh Bilioni 9, licha ya serikali kuwa tayari imeshatoa Sh bilioni 6 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi.

Amesema kusimama kwa mradi huo kumesababisha pia vijana waliokuwa wakitegemea ajira kupitia mradi huo kukosa kipato.

Kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji zilizowasilishwa, mradi huo wa kilomita 7.3 umefikia takribani asilimia 38.5, ambapo kazi zilizokuwa zikiendelea kabla ya kusimama ni pamoja na ulipuaji wa miamba, ujazaji wa kifusi na ujenzi wa makalavati katika maeneo mbalimbali ya mradi.

Iringa Bypass inatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu ya miundombinu katika mji wa Iringa, ikiwa na lengo la kupitisha magari makubwa nje ya katikati ya mji, hasa yale yanayotoka na kuelekea mikoa ya Dodoma, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Kwa miaka mingi, wakazi wa Iringa wamekuwa wakikumbana na changamoto ya msongamano wa magari makubwa katikati ya mji, hali inayosababisha foleni, uchakavu wa miundombinu na wakati mwingine ajali, hususan katika eneo la mlima Ipogolo.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya,  alikiri umuhimu wa mradi huo, akisema ni sehemu ya “mkombozi wa usafiri” kwa mji wa Iringa.

Alieleza kuwa serikali inaendelea kushughulikia masuala ya kifedha ili kuhakikisha mkandarasi analipwa na kurejea kazini kukamilisha ujenzi.

Wakati mjadala huo ukiendelea, wananchi wa Iringa Mjini wameendelea kusubiri kwa hamu kuona kama mradi huo utarejea katika kasi ya ujenzi, huku wengi wakisema kukamilika kwake kutapunguza adha ya usafiri na kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji.

Mradi wa Iringa Bypass ni sehemu ya juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu ya barabara nchini, ikiwa ni mkakati wa kuchochea ukuaji wa uchumi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button