Mavunde: Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini Afrika

DAR ES SALAAM —Serikali imeweka mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji na uongezaji thamani wa madini barani Afrika kupitia uwekezaji mkubwa katika viwanda vya usafishaji, uchakataji na uyeyushaji wa madini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema mkakati huo unalenga kuongeza thamani ya madini yote yanayozalishwa nchini kabla ya kuuzwa katika masoko ya kimataifa, hatua itakayoongeza mapato, ajira na ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC 2026), Mavunde alisema Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Madini na Sera ya Madini ya mwaka 2009 zinazosisitiza uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi.
“Hakuna madini yatakayotoka nje ya nchi bila kuongezwa thamani. Huo ndiyo mwelekeo wa Serikali na tayari wawekezaji wameuelewa,” alisema.
Alisema Tanzania tayari ina viwanda nane vya kusafisha dhahabu na viwanda 16 vya kuongeza thamani ya madini mbalimbali, huku Mkoa wa Dodoma pekee ukiwa na viwanda tisa vinavyojengwa au vilivyoanza uzalishaji.
Aidha, alisema Serikali inaendelea na jitihada za kupata ithibati ya kimataifa ya kiwanda cha kusafisha dhahabu (gold refinery certification), hatua itakayoongeza ushindani wa bidhaa za madini za Tanzania katika soko la dunia.
Mavunde alisema uwekezaji unaendelea pia katika miradi mikubwa ya uchakataji wa madini ikiwemo kiwanda cha kuchakata nikeli na shaba mjini Dodoma, kiwanda cha kuchakata madini ya heavy mineral sands Kigamboni, smelter ya madini inayojengwa Mbeya ambayo itakuwa miongoni mwa nne kubwa duniani, pamoja na utekelezaji wa miradi ya Kabanga Nickel na uchakataji wa uranium.
“Tunataka Tanzania isiwe muuzaji wa malighafi pekee, bali iwe mzalishaji wa bidhaa za madini zenye thamani kubwa zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa mkakati huo unaenda sambamba na kuimarisha ushiriki wa wazawa kupitia sera ya Local Content, ambapo takribani asilimia 90 ya manunuzi ya bidhaa na huduma yenye thamani ya Sh trilioni 5.1 kwa mwaka yanatarajiwa kubaki mikononi mwa kampuni za Kitanzania.
“Wananchi wanapaswa kunufaika si kwa kodi na mrabaha pekee, bali pia kupitia ajira, huduma na ushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini,” alisema.
Kwa mujibu wa Mavunde, mchango wa sekta ya madini umeongezeka kwa kasi baada ya maboresho ya sheria na usimamizi wa sekta hiyo. Mapato ya Serikali kutoka sekta ya madini yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 161 mwaka 2015/16 hadi kufikia Sh trilioni 1.374 mwaka 2025/26 bila kuongezeka kwa idadi ya migodi mikubwa.
Alisema TMIC 2026 utakuwa jukwaa la kutangaza fursa za uwekezaji, kuunganisha wawekezaji na miradi ya kimkakati, kukuza uhamishaji wa teknolojia na ubunifu, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza mchango wa madini katika uchumi wa taifa.



