Utafiti wafichua vikwazo Kilimo cha Mwani

TAFITI zinaonyesha kuwa licha ya wanawake kuwa nguzo kuu ya uzalishaji wa mwani nchini Tanzania lakini bado wanakabiliwa na changamoto zinazopunguza tija na kipato chao.

Utafiti uliofanywa mwaka 2026 kuhusu mnyororo wa thamani wa mwani kwa upande wa Tanzania Bara unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wakulima hawaridhishwi na kiwango cha uzalishaji kutokana na changamoto za masoko, athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa teknolojia na ushiriki mdogo katika maamuzi ya biashara.

Katika utafiti huo, zaidi ya asilimia  70 ya washiriki wa sekta ya kilimo cha mwani wamekuwa wakitumia nguvu zao kufanya  kazi badala ya kumiliki mashamba yao.Unaambiwa asilimia 12 ya wakulima wanaoshiriki shughuli za kuongeza thamani ya zao hilo kutokana na ukosefu wa mitaji, vifaa na ujuzi wa usindikaji.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Robert Eliakim Katikiro anasema: “Ushiriki mkubwa wa wanawake katika uzalishaji haujaambatana na umiliki wa rasilimali, huduma za kifedha na nafasi za kufanya maamuzi, jambo linalopunguza manufaa ya kiuchumi wanayopata.”

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ilibaini kuwa asilimia 94.3 ya wakulima wa mwani hawafanyi shughuli za kuongeza thamani ya mazao yao huku asilimia 82.9 wakiwa hawatunzi kumbukumbu za uzalishaji na zaidi ya nusu wakikosa uelewa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi katika kilimo hicho.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) nchini Tanzania, Dk. Nyabenyi Tito Tipo kupitia taarifa ya mradi wa maendeleo ya sekta ya mwani amesema, “Kuongeza ujuzi wa wakulima, hususan wanawake, katika uzalishaji, usindikaji na biashara ya mwani ni hatua muhimu ya kuongeza kipato na kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 inalenga kuifanya Tanzania iendeleze rasilimali za bahari, maziwa, mito na maeneo mengine ya maji ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi, ajira na ustawi wa wananchi. SOMA: Tabianchi Yatikisa Kilimo cha Mwani

Hatahivyo, Sera hiyo inasisitiza kuimarishwa kwa uratibu wa taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuendeleza shughuli za uchumi wa buluu, ikiwemo uvuvi, ufugaji wa viumbe maji, kilimo cha mwani, usafirishaji wa majini, utalii wa fukwe na bahari, pamoja na uwekezaji unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za maji.

Aidha, sera hiyo inaweka msisitizo katika kukuza utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia, kuongeza thamani ya mazao ya uchumi wa buluu, kujenga uwezo wa wananchi hususan wanawake na vijana, pamoja na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Serikali pia inalenga kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, kuimarisha masoko ya bidhaa zinazotokana na uchumi wa buluu na kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button