Kapinga azindua mabweni mawili Mtwara Girls

MTWARA: WAZIRI wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga, amezindua mradi wa ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari ya Wasichana (Mtwara Girls) iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara unaogharimu zaidi ya Sh milioni 190.
Uzinduzi huo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara kwani amekagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri huyo amesema ujenzi wa mabweni hayo unalenga kuwawezesha wanafunzi hao kupata mazingira salama na rafiki ya kujifunzia na kuishi, hatua inayotarajiwa kuongeza ufaulu.
Aidha, amewahimiza wanafunzi wa shule hiyo kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu na kuwa na mchango katika maendeleo ya taifa.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkuu wa shule hiyo Sikujua Anangisye amesema mabweni hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 160 litalosaidia kuongeza nafasi za wanafunzi wanaoweza kujiunga na shule hiyo.
Aidha, kukamilika kwa mabweni hayo kutasaidia kupunguza changamoto ya malazi kwa wanafunzi na kutoa fursa zaidi kwa wasichana kupata elimu katika mazingira bora.



