Watanzania wakuza uchumi mikopo ya Sh bil 700

DAR ES SALAAM: Maelfu ya Watanzania wameendelea kunufaika na huduma za mikopo zinazotolewa kwa kumiliki pikipiki, bajaji na simu janja kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na mawasiliano.
Hatua hiyo ni baada ya Kampuni ya Watu Credit Tanzania kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 700 ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka mitano ya kampuni hiyo yaliyofanyika Dar es Salaam, Meneja wa Kampuni hiyo, Rumisho Shikonyi, alisema kampuni hiyo imehudumia zaidi ya wateja milioni moja na kupanua huduma zake katika mikoa yote 26 ya Tanzania.
Alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, kampuni imewezesha ununuzi wa pikipiki na bajaji zaidi ya 70,000 pamoja na simu janja zaidi ya milioni 1.5, hatua ambayo imechangia kuongeza fursa za ajira, ujasiriamali na kipato kwa wananchi.
“Miaka mitano iliyopita tulianza tukiwa na lengo la kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia Watanzania wengi zaidi. Leo tumekua na kuwa taasisi inayowezesha wananchi kupata nyenzo muhimu za uzalishaji na kuboresha maisha yao,” alisema Shikonyi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo, Bhavin Parmar, alisema mafanikio ya kampuni katika kipindi hicho yamejengwa katika misingi ya uwajibikaji, uadilifu na ubunifu wa huduma.
Alisema hatua inayofuata ni kuendelea kuboresha huduma kwa kuhakikisha ukuaji wa kampuni unaenda sambamba na maslahi ya wateja, washirika wa biashara, wafanyakazi na jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, utoaji wa huduma unafanyika kwa kutumia teknolojia pamoja na mtandao wa mawakala uliopo katika maeneo mbalimbali nchini, huku wateja wakifanya marejesho ya mikopo kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu na programu ya Watu App.
Mbali na huduma za kifedha, kampuni hiyo imesema imeendelea kuchangia ajira nchini ikiwa na wafanyakazi zaidi ya 500, ambapo wanawake ni takribani asilimia 43 ya nguvu kazi na wanashika karibu nusu ya nafasi za uongozi.
Katika hafla hiyo, kampuni ilitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali, mamlaka za udhibiti, taasisi za kifedha, washirika wa biashara na wateja wake kwa mchango wao katika mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka mitano.
Kampuni hiyo imesema itaendelea kupanua huduma zake kwa kuwekeza zaidi katika teknolojia, kuimarisha ushirikiano na kuongeza upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi.



