Kampuni yakabidhi Sh bil 15 gawio kwa serikali

DAR ES SALAAM: Kampuni Puma Energy Tanzania imekabidhi Serikali ya Tanzania hundi ya gawio la Sh bilioni 15 ambayo ni nusu ya faida iliyopatikana, ikiwa ni gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya kampuni hiyo na kudhihirisha mafanikio ya ushirikiano wake na Serikali kupitia umiliki wa pamoja wa hisa ambapo serikali inamiliki 50 ya hisa hizo.

Gawio hilo lilipokelewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, mbele ya viongozi waandamizi wa Serikali, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Tanzania pamoja na viongozi wa kampuni hiyo. Gawio hilo ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na takribani Sh bilioni 13.5 zilizotolewa mwaka 2025, likionyesha mafanikio makubwa ya kifedha ya kampuni, uwekezaji wa kimkakati na dhamira yake ya muda mrefu ya kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliipongeza kampuni hiyo nakampuni zingine zinazotekeleza wajibu wao kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya taifa na kuonesha manufaa yanayopatikana kupitia ushirikiano madhubuti kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy Tanzania, Balozi George Madafa, alisema gawio hilo la kihistoria linaakisi uimara wa misingi ya biashara ya kampuni pamoja na mafanikio ya mkakati wake wa ukuaji wa muda mrefu.

“Makabidhiano ya gawio la leo yanaakisi utendaji mzuri wa Puma Energy Tanzania, uimara wake na dhamira ya kuendelea kuzalisha thamani endelevu kwa wanahisa wetu na taifa kwa ujumla. Kuongezeka kwa gawio hili kunadhihirisha uimara wa mfumo wetu wa biashara, kujituma kwa wafanyakazi wetu, pamoja na imani ambayo wateja wetu wanaendelea kuiweka kwa kampuni yetu,” alisema Balozi Madafa.

“Kama kampuni inayomilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Puma Energy, tunajivunia kuhakikisha kuwa mafanikio yetu yanawanufaisha moja kwa moja Watanzania kupitia gawio kwa wanahisa, ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali, uwekezaji pamoja na uundaji wa fursa za ajira,” aliongeza Balozi Madafa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema kampuni itaendelea kuunga mkono mabadiliko ya uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji endelevu katika miundombinu ya kimkakati ya nishati pamoja na suluhisho bunifu za nishati.

“Katika miaka ya hivi karibuni, tumewekeza kwa kiwango kikubwa katika kupanua mtandao wetu wa vituo vya huduma, kuimarisha usambazaji wa mafuta ya ndege, kukuza biashara ya gesi ya LPG na kuanzisha matumizi ya nishati safi kama vile Gesi Asilia Iliyobanwa (CNG). Uwekezaji huu unaweka msingi imara wa ukuaji wa baadaye, unaunga mkono ajenda ya nchi ya maendeleo ya viwanda na mabadiliko ya matumizi ya nishati, huku ukiendelea kuhakikisha tunatoa huduma za nishati za kuaminika zinazochangia maendeleo endelevu ya uchumi na ustawi wa Tanzania,” alisema Fatma Abdallah.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya Sh trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali, na pia imetambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na rekodi yake bora ya ulipaji wa kodi na mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Fatma Abdallah.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button