Vijana kunufaika mradi wa Dumisha Amani

SONGEA: Wadau wa mradi wa Dumisha Amani unaotekelezwa na VETA na wamepanga kuanzisha vituo vya vijana (Youth Centres) katika vyuo vya VETA mkoani Mtwara, Lindi, Kigoma na Wilaya ya Songea ili kuwasaidia vijana wenye ujuzi kujiajiri au kuajiriwa.
Mradi huo unafadhiliwa na mashirika ya kimataifa ya UNPDF, UNDP-Tanzania, kampuni ya CPP na GPF-Tanzania
Ofisa Mradi wa Dumisha Amani kutoka UNDP, Josephine Sepeku, ametoa taarifa hiyo Julai 8, 2026 wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa mafunzo kupitia mradi huo, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA Songea.
Sepeku amesema kupitia vituo hivyo vijana watapewa mwongozo na kusaidiwa kuandaa maandiko ya mahitaji ya vitendea kazi wanavyohitaji kulingana na stadi walizopata na kufadhiliwa vitendea kazi ili waweze kuanzisha miradi yao.
Kwa upande wake Ofisa Tarafa ya Muhukuru, Muhammad Maulid Baggo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, amewaomba vijana 60 wanaotarajia kunufaika na mradi huo kuwahamasisha vijana wengine kujiunga katika vyuo vya VETA nchini ili kupata elimu, maarifa na stadi za ufundi ili kuweza kujikwamua kiuchumi lakini pia kujenga jamii yenye amani na utulivu.
“Tuwahamasishe vijana wenzetu kuja VETA kupata elimu ya ufundi stadi ili waweze kunufaika na elimu hii ambayo nyinyi pia mtaipata kupitia mradi huu wa Dumisha Amani,” amesema Baggo.

Sambamba na hilo Baggo amewataka wanufaika hao kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa katika halmashauri ya Manispaa ya Songea na kusema kwamba mikopo hiyo ya asilimia 10 inalenga kunufaisha kundi kubwa la vijana.
“Kwasababu nazungumza na vijana na mmezungumzia maswala ya uwezeshwaji ukiachana na huu mradi wa Dumisha Amani naomba mkawe mabalozi wazuri wa kuwafahamisha vijana kwamba upo mfuko maalumu wa kuwakopesha vijana ambapo manispaa kupitia mapato ya ndani wanawezesha vijana kupata pesa ili kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ili wajikwamue kiuchumi,” ameongeza Baggo.
Kwa upande wake Alphoncina Mshana Afisa Mkuza Mitaala Mwandamizi kutoka VETA Makao Makuu amesema stadi wanazopata wanufaika wa mradi huo zitawawezesha kurudi katika soko la ajira na hivyo kuweza kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine lakini pia wataweza kujipatia kipato sambamba na kuwa mabalozi wazuri wakuhamasisha jamii kulinda na kudumisha amani kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi.
Aidha Mkuu wa chuo cha VETA Songea Rahabu Mwakatundu amesema vijana hao watapatiwa mafunzo katika fani ya Ufundi Umeme, Umeme wa Magari, Ushonaji, Ufundi Bomba na Ufundi Magari.
Mradi wa Dumisha Amani unatekelezwa katika vyuo vya VETA Lindi, Mtwara, Songea na Kigoma na unatarajiwa kuwanufaisha jumla ya vijana 240.



