Sekta binafsi ni chachu ajira kwa vijana – Mzava

Mkuu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ,Godfrey Mzava, amesema serikali itaendelea kutengeneza mazingira bora ya ufanyaji wa shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kwa kutambua kuwa sekta binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa taifa pamoja na uzalishaji wa ajira kwa vijana wa kitanzania.

Mzava amebainisha hayo alipofungua maonesho na Paredi ya wanyama kwenye Maonesho ya 32 ya Wakulima na Wafugaji Nanenane Kanda ya Kaskazini katika viwanja vya Themi- Njiro jijini Arusha na kuongeza kuwa  serikali inatambua sekta hizo kama nguzo za uchumi na ustawi wa wananchi.

“Ninaomba kutoa tena msisitizo wangu katika kutambua mahitaji ya soko kwanza ili kuzalisha kulingana na mahitaji ili kuwa na uhakika wa soko la mazao yetu ya kilimo na ufugaji,sekta binafsi pia niwaeleza kuwa mpo sehemu sahihi na serikali tunatambua mchango wenu katika uchumi na kutengeneza ajira na niahidi kuwa tutaendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji wa shughuli zenu,”amesema.

Akizungumzia Kauli mbiu ya mwaka huu ya “Tambua Soko, Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050”, Mzava amesema utekelezaji wake unapaswa kuanzia kwenye mbegu na namna wakulima na wafugaji wanavyohudumia mashamba na mifugo, masuala ambayo yanapaswa kutekelezwa baada ya kufahamu kile ambacho kimekuwa kikihitajika sokoni.

Akisisitiza kuwa sekta ya Kilimo na ufugaji ndio sekta kubwa zaidi kwa Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, DC Mzava kadhalika amesema lengo la paredi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015 ni kushindanisha wafugaji katika matunzo na ufugaji wenye tija, akibainisha mafanikio ya paredi hiyo ni pamoja na kuongeza uzalishaji na ubora wa mifugo na mazao ya mifugo

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button