Mungu ndiye nguvu ya mafanikio

MSANII wa muziki wa dansi kutoka Twanga Pepeta, Luizer Nyoni Mbutu, amesema hofu ya Mungu na kuongozwa na mafundisho ya Roho Mtakatifu ndiyo siri ya mafanikio yake. Akizungumza na Dailynews Digital jijini Dar-es-salaam, Luizer amesema vijana na jamii kwa ujumla wanapaswa kujifunza kutafuta mafanikio kwa njia halali, kufanya kazi kwa bidii na kuwa na subira.
Amesema tabia ya kutamani mali za wengine na kutaka mafanikio ya haraka imechangia kuporomoka kwa maadili katika jamii. “Kinachoniongoza katika maisha ni hofu ya Mungu na kumsikiliza Roho Mtakatifu. Watu wanapaswa kujifunza kutafuta vyao na kuacha kutegemea mali za wenzao,” amesema.
SOMA: Bella, El Saadat, Twanga Pepeta kukiwasha Valentine Day
Luizer amewataka vijana kuepuka kuiga maisha ya kifahari yasiyoendana na uwezo wao, akisema hali hiyo inaweza kuwasukuma baadhi yao kuingia katika vitendo visivyofaa. Amesisitiza kuwa mafanikio ya kweli yanahitaji juhudi, nidhamu, uvumilivu na kufuata taratibu sahihi, huku akiwataka watu kuridhika na hatua walizofikia na kuendelea kufanya kazi kwa bidii.



