Serikali yaleta mapinduzi huduma za ardhi Mtwara

MTWARA: WANANCHI mkoani Mtwara wameishukuru Serikali kwa kuanzisha huduma za ardhi kwa njia ya kidijitali, hatua inayowawezesha kupata hati miliki kwa urahisi na kupunguza migogoro ya ardhi.
Shukrani hizo zimetolewa wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi Kidijitali uliofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani humo, ambapo wananchi wameelezwa namna ya kutumia mfumo huo kupata huduma za ardhi hata wakiwa nyumbani.
Mmoja wa wananchi walioshiriki uzinduzi huo, Masaida Mussa, amesema mfumo huo umemsaidia kwa kiasi kikubwa, akieleza kuwa hapo awali mchakato wa kupata hati miliki ya ardhi ulikuwa mrefu.
“Kwa kutumia kliniki hii ndani ya siku mbili nimeweza kufanya maombi na hati yangu leo imetoka. Jana nilikuja kuhudhuria mafunzo haya, nikaelekezwa jinsi ya kuingia mtandaoni na kufanya maombi, leo hati imetoka,” amesema Masaida.
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Fratern Hassan, amesema uzinduzi huo umeenda sambamba na utoaji wa huduma za e-Ardhi kwa wananchi.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa njia ya kidijitali na kupunguza ulazima wa wananchi kufuatilia huduma hizo kwa njia za kawaida.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, amesema huduma hiyo kwa sasa inapatikana katika mikoa 17 nchini.
Mikoa hiyo ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Kagera, Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Morogoro.
Amesema wizara hiyo inajipanga kuhakikisha mikoa tisa iliyosalia inaunganishwa na mfumo huo kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2026/2027.



