Ushirikiano wahitajika kupunguza vifo vya uzazi

DAR ES SALAAM: Wadau wa maendeleo wametakiwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya, hususan huduma za uzazi, ili kuongeza usalama wa kina mama na watoto na kupunguza vifo vinavyotokana na changamoto wakati wa ujauzito na kujifungua.
Wito huo umetolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Tibezuka Zinga, wakati wa kupokea msaada wa vifaa vya kujifungulia kutoka Rotary Club ya E-Masaki, ambapo amesema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha huduma za afya, bado hospitali hiyo inakabiliwa na uhitaji wa vifaa kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma.

Amesema ushiriki wa wadau katika sekta ya afya ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na kuimarisha mazingira ya utoaji huduma, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto zinazowakabili kina mama wakati wa kujifungua na hatimaye kuokoa maisha yao pamoja na watoto.
Kwa upande wake, Rais wa Rotary Club ya E-Masaki, Shehzada Amir, amesema klabu hiyo imeamua kutoa msaada huo baada ya kubaini uhitaji wa vifaa katika hospitali hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi.

Amesema wanaamini kuwa mchango huo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifungulia na kuwawezesha watumishi wa afya kutoa huduma bora na salama kwa kina mama na watoto, huku akieleza kuwa klabu hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wengine katika kusaidia mahitaji ya jamii.



