Serikali yazindua mwongozo elimu ya fedha kwenye mitaala

DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amezindua rasmi Mwongozo wa Kuchopeka Elimu ya Fedha katika Mitaala ya Elimu ya Juu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania, ukiwa na lengo la kuwezesha wanafunzi na wahitimu kufanya maamuzi sahihi na yenye uwajibikaji kuhusu fedha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo leo jijini Dar es Salaam, Wanu amesema elimu ya fedha ni muhimu katika maendeleo ya rasilimali watu, hasa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kupitia teknolojia za kidijitali.
“Elimu ya fedha inapaswa kuwa ajenda yetu muhimu ya maendeleo ya rasilimali watu ili kuwawezesha vijana kufanya maamuzi sahihi,” amesema.
Amesema mwongozo huo unalenga kuhakikisha mitaala inaakisi elimu ya fedha, wanafunzi wanapata ufundishaji na upimaji unaojenga umahiri na kutumia maarifa hayo katika maisha ya kila siku.
Aidha amesema wahitimu wanapaswa kuwa na uwezo wa kupanga na kusimamia mapato na matumizi, kuweka akiba, kukopa kwa uwajibikaji, kuelewa fursa na athari za uwekezaji, kujikinga na udanganyifu wa kifedha pamoja na kutumia teknolojia za kifedha kwa usalama.
“Haitoshi kuwa na wahitimu wenye shahada, stashahada na vyeti pekee, bali tunahitaji wahitimu wenye maarifa, ujuzi, umahiri, ubunifu na maadili mema,” amesema.
Pia, amezitaka TCU na NACTVET kuhakikisha elimu ya fedha inazingatiwa katika vigezo vya udhibiti wa ubora, huku taasisi za fedha, sekta binafsi na washirika wa maendeleo zikihimizwa kushirikiana na vyuo katika mafunzo ya vitendo na programu za ujasiriamali.
Amesema uzinduzi huo ni mwanzo wa utekelezaji wa mwongozo huo ambao unalenga kujenga kizazi cha wahitimu wenye uwezo wa kifedha unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



