SUA yaanza utekelezaji agizo la makamu wa rais

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanza kutekeleza agizo la Makamu wa Rais la kuwawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu wa kazi kwa kuwaunganisha wanafunzi na wahitimu wa chuo hicho wanaoongoza kampuni na taasisi mbalimbali.
Hatua hiyo inalenga kuwapa wanafunzi na wahitimu fursa ya kujifunza kutoka katika mazingira halisi ya kazi, ikiwemo uzalishaji, uendeshaji wa biashara na shughuli nyingine zinazohusiana na mahitaji ya soko la ajira.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu), Profesa Maulid Mwatawala, amesema hayo wakati wa kikao na viongozi wa kampuni waliohitimu SUA, kilichoandaliwa na Kitengo cha Umataifishaji na Majalisi chuoni hapo.
Amesema kikao hicho kililenga kujadili fursa za ushirikiano kati ya SUA na wahitimu wa chuo hicho wenye kampuni, hususan namna ya kuwapatia wanafunzi na wahitimu ujuzi unaoendana na mazingira halisi ya kazi na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa mujibu wa Profesa Mwatawala, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais yanayosisitiza umuhimu wa vijana 10,000 kupata ujuzi na uzoefu wa kazi kila mwaka.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais alitoa maelekezo na sisi kama taasisi yalitufikia kupitia CEO ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo. Makamu wa Rais aliagiza TCU, ndiyo mdhibiti wetu anayetusimamia, anahitaji kuona vijana 10,000 wakipata ujuzi na uzoefu wa kazi kila mwaka. Mafunzo kwa vitendo yanahitajika ili kupata huo ujuzi,” amesema.

Amesema SUA imeamua kulibeba mapema suala hilo kupitia jukwaa linalowakutanisha viongozi wa kampuni waliohitimu chuoni hapo kwa ajili ya kujadili fursa mbalimbali za maendeleo ya chuo na namna ya kuwaunganisha wanafunzi na mazingira halisi ya kazi.
Profesa Mwatawala amewataka viongozi hao kutumia nafasi walizonazo kuwawezesha wanafunzi wa SUA kupata uzoefu wa vitendo kupitia miradi na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika taasisi na kampuni zao.
“Ninawasihi viongozi (Ma CEO) wa kampuni mliohitimu SUA, tumieni nafasi zenu kuwapa wanafunzi wetu fursa za kupata uzoefu wa vitendo kupitia miradi na shughuli mbalimbali kwenye taasisi zenu na kampuni,” amesema.
Amesema fursa hizo zinaweza kujenga daraja kati ya maarifa yanayopatikana darasani, ujuzi wa vitendo na uzoefu wa kazi, hatua ambayo inaweza kuongeza uwezekano wa vijana kupata ajira au kujiajiri.
Kabla ya kuanza kwa jukwaa hilo, viongozi hao walifanya ziara ya kutembelea shughuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa na SUA kwa lengo la kupata uelewa wa shughuli za chuo na kubaini maeneo ya ushirikiano.
Katika ziara hiyo, walijifunza kuhusu utekelezaji wa Mradi wa APOPO na kutembelea eneo kinapojengwa kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za SUA, ikiwemo maji na sharubati.
Pia walitembelea majengo yanayotekelezwa kupitia Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET).
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara kutoka Benki ya NMB Makao Makuu, Nsolo Mlozi, ambaye ni mhitimu wa SUA, amesema benki hiyo imetenga Sh bilioni 20 kwa ajili ya kuendeleza miradi anzilishi ya vijana na makundi maalum.
Mlozi amesema uwezeshaji wa miradi hiyo una umuhimu katika kukuza uchumi wa Taifa, huku ukiwapa wahitimu fursa ya kupata uzoefu katika uzalishaji na uendeshaji wa biashara.
“Miradi anzilishi pamoja na kuchangia katika uchumi wa Taifa, pia inasaidia wahitimu kupata uzoefu katika uzalishaji na uendeshaji wa biashara,” amesema.


