GEITA: WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kuweka taa 400 za barabarani ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Geita  na maeneo mengine mkoani Geita kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2026/27.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita, Mhandisi Hosea Machaka, ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari na kueleza mpango wa kuweka taa hizo umetekelezwa kati ya Septemba hadi Oktoba 2026

Mhandisi Machaka amesema dhamira ya kuweka taa hizo ni kuimarisha usalama wa madereva, watembea kwa miguu na wafanyabiashara nyakati za usiku ili kupunguza ajali za barabarani na matukio ya uharifu.

Amesema taa za barabarani ni muhimu hasa katika kipindi cha msimu wa mvua, kwa kuwa zinasaidia madereva kuona vizuri na hivo kuongeza usalama kwenye barabara yenye matumizi makubwa ya magari.

Ameongeza, pia uwekaji wa taa hizo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupitia TANROADS wa kupendezesha miji, kuimarisha usalama na kuchochea shughuli za kiuchumi na usafirishaji wakati wa usiku.

Aidha, Mhandisi Machaka amewataka wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda na kutunza miundombinu ya barabara ikiwemo taa hizo ili kuchochea ubora wa huduma na usalama wa barabarani na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake mjasiriamali na mkazi wa Shilabela, Peter Kulwa, amesema taa hizo zimebadili mazingira ya biashara eneo hilo, akieleza kuwa awali walilazimika kufunga biashara mapema kutokana na giza.

“Toka tuanze kufanya biashara hapa, kipindi cha nyuma tulikuwa tunafanya biashara kwa giza kwa sababu barabara ilikuwa haina mataa, ila tangu yawekwe mataa saivi tunafanya biashara vizuri,” amesema Kulwa.

Amesema kutokana na uwepo wa taa hizo, sasa anaweza kuuza matunda kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 5 au saa 6  usiku, tofauti na awali ambapo biashara zilimalizika majira ya saa 3 usiku.

Naye, Ofisa Usafirishaji, Novatus Amin amesema taa hizo zimeondoa changamoto ya kufanya kazi na kutembea gizani na kukaa kwenye maegesho wakati wa usiku bila hofu tofauti na hapo awali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button