Wazazi watakiwa kuweka mkazo malezi ya watoto

IRINGA: WAZAZI na walezi wametakiwa kutambua kuwa mafanikio ya watoto hayaishii katika kupata elimu darasani, bali yanategemea pia malezi yanayojenga maadili, nidhamu na uwajibikaji katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Mount Komaguru, Dk Yahaya Msigwa, wakati wa mahafali ya nne ya shule hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha elimu na malezi bora katika kuwajenga vijana wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakielekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha watoto wanasoma, huku wakitoa kipaumbele kidogo kwa malezi, hali inayoweza kuathiri mwenendo wao na namna wanavyoshirikiana na jamii.

Dk Msigwa amesema watoto wanahitaji kuandaliwa kitaaluma na kimaadili ili waweze kutumia elimu wanayoipata kwa manufaa yao binafsi na maendeleo ya taifa, huku wakiheshimu tamaduni na misingi inayokubalika katika jamii ya Kitanzania.
Ameeleza kuwa jukumu la kuwajenga watoto si la walimu pekee, bali linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya shule, wazazi na walezi ili kuhakikisha vijana wanakua katika mazingira yanayowasaidia kuwa raia wema na wenye kuwajibika.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa shule hiyo, Baraka Kapesa, amewataka wahitimu wa kidato cha nne kuendeleza misingi ya maadili waliyojifunza shuleni na kuitumia elimu yao kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika familia na jamii zinazowazunguka.
Kapesa amesema wahitimu wanapaswa kutambua kuwa kuhitimu masomo ni hatua muhimu katika safari yao ya elimu na maisha, hivyo wanapaswa kuendelea kuwa na nidhamu na kufanya maamuzi yanayozingatia mustakabali wao.
Katika risala iliyosomwa kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Mpwira Mwaletelo ameiomba jamii kuzingatia changamoto zinazokabili shule hiyo, akitaja ukosefu wa pampu ya maji kuwa kikwazo katika shughuli za umwagiliaji.
Amesema upatikanaji wa pampu hiyo utasaidia kurahisisha shughuli za umwagiliaji na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za kilimo zinazofanyika shuleni.

Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Mkaguzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kilolo, Robert Mahundi, amewataka wazazi kuunga mkono ufundishaji wa somo la kilimo mashuleni ili wanafunzi wapate ujuzi unaoweza kuwasaidia hata baada ya kumaliza masomo.
Mahundi amesema kilimo kinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujitegemea kiuchumi kwa vijana iwapo watawezeshwa kupata maarifa na kuyatumia katika shughuli za uzalishaji.
Amehimiza ushirikiano kati ya wazazi na shule katika kuendeleza elimu ya kilimo, akieleza kuwa ujuzi huo unaweza kuwasaidia vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na kuboresha maisha yao.
Katika mahafali hayo, wanafunzi 22 wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, hatua inayoweka mkazo katika maandalizi yao ya kuhitimisha ngazi hiyo ya elimu na kuendelea na hatua nyingine za maisha.



