Teknolojia mpya kubaini maeneo yaliyokosa umeme

ARUSHA: Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imebuni teknolojia inayoweza kubaini maeneo ambayo umeme umekatika kwenye gridi ya taifa, ikiwa katika hatua za kuhakiki na kuthibitisha ufanisi wake kabla ya kuanza kutumika kwa upana zaidi.

Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema teknolojia hiyo itarahisisha kazi za wahandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa kuwa wataweza kutambua maeneo yaliyoathirika kupitia kompyuta bila kulazimika kwenda kutafuta hitilafu eneo kwa eneo.

Amesema teknolojia hiyo inaweza pia kutumika katika ngazi ya kaya, ambapo mtumiaji ataweza kutumia simu ya mkononi kubaini iwapo kukatika kwa umeme kunatokana na hitilafu katika eneo lake. Hatua hiyo inatarajiwa kurahisisha utambuzi wa hitilafu na kuharakisha urejeshwaji wa huduma.

Profesa Kipanyula amesema ili teknolojia hizo ziweze kutumika kwa ufanisi na kuwafikia wananchi wengi, zinahitaji kuungwa mkono na takwimu sahihi zitakazosaidia kupima na kuthibitisha matokeo yake.

Amesema kutokana na umuhimu wa takwimu katika kuendeleza ubunifu na kutatua changamoto za jamii, NM-AIST imesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), kwa lengo la kuunganisha utaalamu wa sayansi, teknolojia na ubunifu na ujuzi wa takwimu.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia pia kuendeleza teknolojia za kubaini maeneo yanayopoteza maji katika mifumo ya usambazaji, ili kurahisisha utambuzi wa changamoto na kuboresha huduma kwa wananchi.

Profesa Kipanyula amesema lengo la NM-AIST si kuzalisha ubunifu pekee, bali kuhakikisha teknolojia zinazobuniwa zinafikia soko na kutumiwa na wananchi katika kuboresha huduma na kuongeza tija.

Kwa upande wake, Mkuu wa EASTC, Profesa Tumaini Katunzi, amesema takwimu ni msingi muhimu wa kupima maendeleo ya taifa na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Amesema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na NM-AIST utasaidia kuongeza matumizi ya takwimu na ushahidi wa kisayansi katika kufanya maamuzi, pamoja na kuibua suluhisho za kiteknolojia zinazokidhi mahitaji halisi ya jamii.

Profesa Katunzi amesema makubaliano hayo yanahusisha maeneo mbalimbali, yakiwemo ufundishaji, kufanya tafiti kwa pamoja na kubadilishana maarifa, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa taasisi hizo kuzalisha maarifa na teknolojia zenye manufaa kwa maendeleo ya taifa.

Amesisitiza kuwa matumizi ya takwimu sahihi yatasaidia taasisi na mamlaka husika kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kutumia ushahidi, badala ya kutegemea makadirio pekee.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button