Madaktari Tanzania watoa huduma za kibingwa Malawi

MALAWI: Timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) nchini Tanzania imehitimisha kambi ya matibabu ya kibingwa nchini Malawi, ambapo wagonjwa 64 wamefanyiwa upasuaji na wengine 49 kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa matibabu zaidi.
Kambi hiyo imefanyika chini ya ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Malawi katika sekta ya afya, ikiwa na lengo la kutoa huduma za matibabu ya kibingwa pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi kati ya wataalamu wa afya wa nchi hizo mbili.

Akifunga kambi hiyo, Katibu Mkuu wa Utawala wa Wizara ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Malawi, Bestone Chisamile, amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa ikitekeleza kwa vitendo ushirikiano wa matibabu ya kibingwa kati ya nchi hizo.
“Ushirikiano wa afya kati ya Malawi na Tanzania unatekelezwa kupitia kambi ya matibabu ya kibingwa nchini Malawi. Hata hivyo, tumeanza majadiliano yatakayolenga kuangalia manufaa ya kambi hiyo kwa wagonjwa pamoja na umuhimu wa kurasimisha ushirikiano mpana zaidi unaojumuisha huduma za matibabu, mafunzo ya wataalamu, masuala ya dawa na rufaa za wagonjwa,” amesema Chisamile.

Amesema madaktari na wataalamu kutoka Tanzania wameleta ujuzi na uzoefu katika fani mbalimbali za matibabu na kubadilishana maarifa na wenzao wa Malawi katika Hospitali ya Mzuzu na Hospitali ya Kamuzu, Lilongwe.
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Agnes Kayola, amesema kambi hiyo imekuwa fursa kubwa kwa wananchi wa Malawi kupata huduma za matibabu ya kibingwa, huku wataalamu wa afya wa nchi hizo mbili wakinufaika kupitia kubadilishana uzoefu.
“Kambi hii imewanufaisha wagonjwa zaidi ya 810, ambapo 64 wamefanyiwa upasuaji na 49 wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa. Faida nyingine ya kambi hii ni kuwezesha wataalamu wa afya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma kati ya nchi hizi mbili,” amesema Balozi Kayola.
Kambi hiyo ilianza Septemba 28, 2026 na imehitimishwa Oktoba 10, 2026, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), SOTAC na MSD.
Aidha, kambi hiyo ilitumia magari maalumu yenye vyumba vya kisasa vya upasuaji, vilivyowezesha wataalamu kutoa huduma za matibabu katika mazingira mbalimbali.



