SUA kuimarisha afya ya wanyama

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatarajia kutumia maadhimisho ya miaka 50 ya ufundishaji wa taaluma ya udaktari wa mifugo nchini kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya wanyama, kuongeza uelewa kwa wafugaji na kutathmini mchango wa tafiti katika sekta hiyo.
Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda, amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo yamepangwa kuanza Novemba 22, hadi 27, mwaka huu.
Katika maadhimisho hayo, Chuo kimeandaa shughuli mbalimbali zitakazohusisha utoaji wa huduma za matibabu ya wanyama bure, kongamano la kisayansi, maonesho pamoja na mbio za hisani.
Amesema kutakuwepo na utoaji wa huduma za uchunguzi na tiba za Wanyama ,na zaidi ya madaktari 300 wa mifugo watashiriki katika Manispaa ya Morogoro na Wilaya ya Mvomero.
Amesema huduma zitakazotolewa ni uchunguzi, matibabu, upasuaji na ushauri wa kitaalamu kwa wafugaji bila malipo kwa wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo ,pia mbwa na paka.
Profesa Chibunda amesema watatoa huduma mbalimbali zikiwemo za uzazi wa mpango kwa Wanyama kama Mbwa na lengo ni kwa kuwasaidia wafugaji kukabiliana na changamoto zinazowakabili”alisema Profesa Chibunda.
Amesema maadhimisho hayo ya miaka 50 ni tangu Serikali ilipoanzisha mafunzo ya udaktari wa mifugo nchini mwaka 1979, baada ya awali Watanzania wachache kupelekwa kusomea taaluma hiyo katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya.
Profesa Chibunda amefafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa mafunzo hayo, SUA imezalisha wahitimu takribani 1,580 ambao wanahudumia sekta ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Amesema kwa kipindi hicho, chuo hicho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika kudhibiti magonjwa ya wanyama, kulinda afya za mifugo na wanyamapori pamoja na kuhakikisha usalama wa bidhaa zitokanazo na wanyama.
Profesa Chibunda amesema,Makamu wa Rais anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuzindua mnara wenye majina ya wanafunzi wote waliowahi kusoma katika programu ya udaktari wa mifugo chuoni hapo.
Amesema Makamu wa Rais pia ataweka jiwe la msingi kati ya majengo matano makubwa yanayojengwa na Chuo baada ya kupata fedha Sh bilioni 73 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Amesema fedha hizo zimewezesha ujenzi wa madarasa, kumbi za mihadhara na mabweni katika kampasi za chuo hicho, ikiwemo Kampasi ya Mizengo Pinda na Kampasi ya Solomon Mahlangu.
Profesa Chibunda amesema uwekezaji huo unalenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia pamoja na kuongeza uwezo wa chuo kutoa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika nchini.
Kwa upande wake Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya , Profesa Esron Karimuribo ,amesema Chuo kimeandaa kongamano la kisayansi litakalowakutanisha wataalamu, watafiti na wadau wa sekta ya mifugo kutoka ndani na nje ya nchi kujadili mafanikio ya tafiti zilizofanyika katika kipindi cha miaka 50 na namna zinavyoweza kutatua changamoto za jamii.
Amesema kuanzia Novemba 24 hadi 27,yatafanyika maonesho viwanja vya Kampasi ya Edward Moringe yatakayotoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu ufugaji bora, udhibiti wa magonjwa na huduma mbalimbali zinazotolewa katika mnyororo wa thamani wa kilimo mifugo.



