Je, vyakula vya asili suluhisho magonjwa yanayoongezeka?

DAR ES SALAAM: Vyakula vilivyokuwa sehemu ya maisha ya kila siku katika jamii za Kitanzania sasa vinaingia kwenye mjadala wa kisayansi, huku wataalamu wakichunguza mchango wake katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
Kiburu, mchanganyiko wa maharage na ndizi, mazao ya mizizi na mbege, kinywaji kinachotengenezwa kwa kuchachusha ulezi na ndizi, ni miongoni mwa vyakula vya asili vinavyochunguzwa ili kuelewa mchango wake katika afya ya binadamu.

Mjadala huo unakuja wakati mifumo ya ulaji nchini ikibadilika kutokana na ukuaji wa miji, utandawazi na ongezeko la vyakula vilivyosindikwa viwandani.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, aliyesema Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili za lishe, ikiwemo kuendelea kuwepo kwa udumavu na upungufu wa virutubisho, huku unene, uzito uliopitiliza na magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo yakiongezeka.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi la Mpango wa Lishe Duniani (World Diet Initiative) jijini Dar es Salaam, Profesa Sunguya alisema kukabiliana na hali hiyo kunahitaji kuangalia zaidi ya matibabu na kuelekeza nguvu kwenye sababu za msingi, ikiwemo ulaji usiofaa na mabadiliko ya mazingira ya chakula.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa vyakula vya asili havitoi kinga dhidi ya magonjwa moja kwa moja, akitaka kufanyika kwa tafiti za kina kuhusu virutubisho vyake, mbinu za uandaaji na uwiano sahihi wa mlo kabla ya kuingizwa katika sera za afya ya umma.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Sabina Mugusi, alisema ukuaji wa miji, utandawazi na ongezeko la vyakula vilivyosindikwa viwandani vinabadilisha kwa kasi mifumo ya ulaji nchini.
Aliwahimiza watafiti kuziba pengo kati ya tafiti na jamii kwa kubadilisha matokeo ya maabara kuwa suluhu za vitendo zinazozingatia utamaduni wa wenyeji na gharama nafuu.
Profesa Mugusi aliongeza kuwa kongamano hilo linalenga kuweka ajenda ya pamoja ya utafiti wa kimataifa ili kuhifadhi urithi wa mapishi unaotoweka na kuongoza mikakati endelevu ya lishe barani Afrika na kwingineko.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha KCMC, Dk. Godfrey Temba, alisema matokeo ya awali ya utafiti wa miaka saba uliofanyika mkoani Kilimanjaro yanaonyesha kuwa vyakula vikuu vya asili vina uwezo mkubwa wa kulinda afya.
Alivitaja kiburu, mazao ya mizizi na mbege kuwa na vimelea hai vyenye manufaa na virutubisho muhimu vinavyoweza kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza hatari ya magonjwa sugu.

Kongamano hilo lililoandaliwa na MUHAS limewakutanisha wanasayansi, watunga sera na wataalamu wa afya ya jamii kutoka zaidi ya mataifa 16.



