Ndejembi ataja faida matumizi nishati safi ya kupikia

LINDI:MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaweza kupunguza athari za moshi kwa afya za wananchi, kulinda mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati katika kaya.
Amesema matumizi ya gesi badala ya kuni na mkaa yatasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na athari za kiafya zinazotokana na kuvuta moshi wakati wa kupika.
Ndejembi ameyasema hayo wakati wa zoezi la ugawaji wa sehemu ya mitungi 750 ya gesi yenye ujazo wa kilo sita kwa wananchi wa Jimbo la Mchinga, mkoani Lindi. Mitungi hiyo imetolewa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Lake Gas, chini ya Lake Group, na Mbunge wa jimbo hilo, Salma Kikwete.
Amesema kuhamasisha matumizi ya nishati safi ni sehemu ya hatua za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambazo matumizi yake yanaweza kuathiri afya za watumiaji na mazingira.
“Mitungi hii ya gesi na nishati safi ya kupikia inaenda kulinda afya zetu. Badala ya kupika kwa kutumia mkaa na kuvuta moshi wote unaotokana na upishi, sasa tunaenda kutumia nishati safi ambayo haitadhuru afya zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa matumizi ya gesi yanaweza kusaidia kaya kupunguza gharama za upishi ikilinganishwa na matumizi ya mkaa.
Awali, Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete, amesema mitungi hiyo imepatikana kupitia ushirikiano wake na kampuni ya Lake Gas, ambao umewezesha wananchi kupata vifaa vya kuanzia kutumia nishati hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Lake Gas Tanzania, Sadiq Sabri, amesema kampuni hiyo imeshirikiana na mbunge huyo kugawa mitungi 750 yenye ujazo wa kilo sita kwa wananchi wa jimbo hilo.
Amesema ushiriki wa kampuni hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo lengo la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Zoezi hilo limefanyika wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan kwa kaya ambazo bado zinatumia kuni na mkaa.



