KCMC yaweka nguvu zaidi vipimo vya maabara

KILIMANJARO; Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro inatarajia kuongeza zaidi ya vipimo vipya 40 katika huduma zake za maabara, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa uchunguzi wa magonjwa, kuongeza kasi ya upatikanaji wa majibu na kupunguza uhitaji wa kupeleka sampuli za wagonjwa katika maabara za nje ya nchi.

Akizungumza  wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Kimataifa la Hospital Partnership Alliance (HPA Global Forum 2026), linaloendelea kufanyika katika hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga, Mkurugenzi wa KCMC, amesema hospitali hiyo inaendelea kupanua miundombinu ya maabara na kuongeza uwezo wa kufanya vipimo mbalimbali ili huduma nyingi muhimu za uchunguzi zipatikane ndani ya hospitali hiyo.

Amesema kukamilika kwa mpango huo kutapunguza utegemezi wa maabara za nje ya nchi, kurahisisha upatikanaji wa majibu ya vipimo na kuwawezesha madaktari kufanya maamuzi sahihi ya matibabu kwa wakati, jambo litakaloongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Ameeleza kuwa miongoni mwa manufaa yanayotarajiwa kutokana na upanuzi huo ni kuimarika kwa uwezo wa wataalamu wa KCMC kutambua mapema magonjwa hatari ya mlipuko kama Ebola, kabla hayajasambaa zaidi, kupitia matumizi ya vifaa na teknolojia za kisasa za maabara pamoja na utaalamu wa wataalamu wa hospitali hiyo.

Amesema ushirikiano kati ya KCMC na Hospital Partnership Alliance (HPA) ni miongoni mwa nguzo zilizochangia kukamilika na kuimarika kwa huduma za maabara hiyo.

Kupitia muunganiko huo, KCMC imepata fursa ya kushirikiana na taasisi mbalimbali za afya, kubadilishana utaalamu na kupata maarifa na uzoefu unaosaidia kuimarisha uwezo wa kufanya vipimo na kutoa huduma bora za uchunguzi.

“Ushirikiano huo pia unaweka msingi wa kuendelea kupanua uwezo wa maabara na kuimarisha huduma za afya kwa kutumia teknolojia na utaalamu kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano huo, Dk Jeremya Piuza, mtaalamu wa Idara ya Patholojia KCMC na mwanachama wa HPA, amesema mtandao huo unaunganisha hospitali zenye uwezo na maeneo tofauti ya ubobezi ili ziweze kushirikishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa wataalamu wa mataifa mengine.

Amesema kupitia ushirikiano huo, hospitali za Tanzania zinaweza kujifunza kutoka kwa taasisi zenye uzoefu mkubwa katika maeneo mbalimbali ya kitabibu, huku nazo zikitoa utaalamu wake katika maeneo ambayo zimeendelea kufanya vizuri.

 

Ametoa mfano wa KCMC kuwa na uzoefu katika eneo la magonjwa ya kuambukiza, jambo linaloweza kuwawezesha wataalamu kutoka hospitali nyingine kujifunza kutoka kituoni hapo. Wakati huo huo, wataalamu wa Tanzania wanapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzao wenye uzoefu mkubwa katika magonjwa ya figo, moyo na maeneo mengine ya kitabibu.

Amesema HPA pia hutumia teknolojia za kidijitali kuwaunganisha wataalamu waliopo katika mataifa tofauti, hali inayomwezesha daktari kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mtaalamu mwingine kuhusu changamoto ya mgonjwa bila kulazimika kusafiri.

Ameongeza kuwa mtandao huo unalenga kuimarisha ufadhili wa tafiti zinazotafuta majibu ya changamoto zinazoathiri jamii, ikiwemo kubaini visababishi vya homa zisizotokana na malaria. Tafiti hizo zitasaidia kupata ushahidi wa kisayansi utakaoboresha mbinu za kuzuia, kutambua na kutibu magonjwa mbalimbali.

Kwa upande wake, Dk Helga Mutasingwa, mwakilishi wa St Trizza Health Network Tanzania, amesema HPA ni jukwaa linalowaunganisha wataalamu wa afya, hospitali, taasisi za elimu, mashirika na wadau wengine kutoka zaidi ya nchi 30 duniani.

Amesema ushirikiano huo unatoa nafasi kwa nchi kujifunza kutoka kwa nyingine, kubadilishana wataalamu na wanafunzi, pamoja na kuendesha tafiti za pamoja ambazo matokeo yake yanaweza kutumika kuboresha sera na miongozo ya afya.

Ameeleza kuwa changamoto nyingi zinazokabili mifumo ya afya zinafanana licha ya nchi kutofautiana kiuchumi na kiteknolojia, hivyo kuunganisha uzoefu na uwezo wa kila nchi kunaweza kusaidia kupata suluhisho lenye manufaa mapana zaidi.

Dk Mutasingwa amesema matarajio mengine ya ushirikiano huo ni kuimarisha ufadhili wa ndani wa sekta ya afya, matumizi ya akili mnemba (AI), uvumbuzi wa kiteknolojia na kuongeza uwezo wa wataalamu kupitia mafunzo na miradi ya pamoja.

Amesisitiza kuwa sekta ya afya haiwezi kuendelea kwa kutegemea juhudi za nchi moja pekee, bali inahitaji ushirikiano unaowezesha wataalamu kushirikishana maarifa na rasilimali ili kukabiliana na changamoto zinazovuka mipaka ya mataifa.

Jukwaa hilo, ambalo bado linaendelea, linatoa fursa kwa KCMC na taasisi nyingine za afya kutoka nchi mbalimbali kubadilishana uzoefu, utaalamu na teknolojia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button