Tanzania, Nordic zajadili AI kuboresha mifumo ya afya

DAR ES SALAAM: Tanzania na nchi za Nordic zimejadili fursa za matumizi ya Akili Mnemba (AI) na teknolojia bunifu katika kuboresha mifumo ya afya, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kupima usalama, ubora na ufanisi wa teknolojia hizo kabla ya kuziingiza katika matumizi ya jamii.
Nchi hizo ni Sweden. Finland, Norway, Denmark ambazo zote kwa pamoja zimekubali kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kuboresha mifumo ya afya kwa kutumia teknolojia za AI.

Akizungumzia usimamizi wa bunifu hizo, Mkuu wa Sehemu ya Maboresho ya Sekta ya Afya, Dk. Vivian Wonanji, amesema Serikali hutumia utafiti wa majaribio (pilot study) kupata ushahidi kuhusu ubora, ufanisi na kukubalika kwa teknolojia kwa watumiaji, huku uendelevu wake ukizingatiwa tangu hatua za mwanzo.
“Hatuwezi kuanzisha teknolojia ambayo baadaye inaweza kuleta madhara au kushindwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa,” amesema Wonanji.
Amesema Serikali pia huhakikisha wadau muhimu wanashirikishwa tangu mwanzo wa mchakato, wakiwemo Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, washirika wa maendeleo, wataalamu wa sekta husika, taasisi za elimu ya juu na utafiti pamoja na wananchi watakaonufaika na teknolojia hizo.

Ameeleza kuwa ushirikishwaji huo unasaidia kupata ushahidi na taarifa kutoka kwa makundi mbalimbali, hivyo kuiwezesha Serikali kufanya maamuzi sahihi kuhusu bunifu zinazofaa kuendelezwa na kutumika.
Akitolea mfano, amesema STA imeandaa programu tumizi rahisi yenye moduli takribani 13 zinazowasaidia watoa huduma katika maeneo mbalimbali, akieleza kuwa huo ni mfano wa namna Serikali inavyosimamia upokeaji wa bunifu mpya.
Mjadala wa Tanzania na nchi za Nordic umejikita katika mfumo wa ushirikiano wa sekta nne, Quadruple Helix Model, unaounganisha Serikali, vyuo vikuu na taasisi za utafiti, sekta binafsi pamoja na jamii katika kuzalisha na kuendeleza suluhisho za kiteknolojia.

Kupitia mada ya Collaborate to Innovate: Nordic-Tanzanian Perspectives on the Quadruple Helix Model, washiriki wamejadili namna ya kuunganisha maarifa ya kitaaluma, uwekezaji, sera na mahitaji ya wananchi ili kuhakikisha bunifu zinazozalishwa zinatatua changamoto halisi katika sekta ya afya.
Matumizi ya AI yanafungua fursa katika uchambuzi wa taarifa za wagonjwa, kusaidia utambuzi wa magonjwa, kuboresha usimamizi wa hospitali na kuwawezesha wataalamu wa afya kufanya maamuzi yanayotegemea taarifa sahihi.
Katika kuhakikisha teknolojia hizo zinakuwa endelevu na zinawanufaisha wananchi, Wonanji amesema Serikali inalenga kutumia bajeti za umma na mfumo wa bima ya afya kugharamia teknolojia zenye manufaa kwa wananchi badala ya kutegemea kwa muda mrefu ufadhili wa washirika wa maendeleo.

Amesema teknolojia zinazostahili zinapaswa kuingizwa katika vifurushi vya bima ya afya ili gharama zake ziweze kulipwa kupitia mfumo huo, huku nyingine zikigharamiwa kupitia bajeti za Serikali na mfumo wa ununuzi wa vifaa tiba unaosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD).
Ameeleza kuwa mkakati huo unalenga kupunguza utegemezi wa malipo ya moja kwa moja kutoka kwa wagonjwa na kuhakikisha kila teknolojia mpya ina mpango endelevu wa kugharamiwa na kuingizwa katika mfumo wa kawaida wa bajeti za Serikali.
Kwa Tanzania, ushirikiano huo na nchi za Nordic unatoa fursa ya kuimarisha uwezo wa taasisi za ndani katika utafiti, kukuza ubunifu na kutengeneza suluhisho zinazozingatia mazingira na changamoto za mfumo wa afya nchini.
Changamoto kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa hazibaki katika majaribio au tafiti za kitaaluma, bali zinabadilishwa kuwa huduma salama, zinazofikika na zenye manufaa kwa wananchi.
Kwa msingi huo, ushirikiano wa Tanzania na nchi za Nordic unaweza kuchangia kuharakisha mageuzi ya sekta ya afya kupitia matumizi ya teknolojia, utafiti, uwekezaji na mifumo endelevu.
Profesa Sabina Mugusi, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha bunifu zinazofanyika katika sekta ya afya zinavuka hatua za utafiti na majaribio na kuanza kutumika kuwahudumia wananchi.
Amesema Serikali inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kugharamia bunifu hizo kupitia mgao wa fedha katika bajeti ya taifa, huku ikishirikisha mifumo ya bima ya afya na washirika wa maendeleo kuongeza nguvu ya kifedha.

Profesa Mugusi pia amesisitiza umuhimu wa kuweka mikakati ya ununuzi wa teknolojia za afya kulingana na mahitaji ya sekta hiyo, pamoja na kuongeza uzalishaji na uunganishaji wa teknolojia hizo nchini.
Amesema hatua hizo zitasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuimarisha uwezo wa Tanzania kugharamia, kuzalisha na kuendeleza bunifu zake za kiteknolojia katika sekta ya afya.
Johan Müllern-Aspegren, Mkuu wa Kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii na Kiongozi wa Masuala ya Teknolojia Zinazochipukia katika kampuni ya Capgemini Sweden, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden katika kukuza ubunifu wa teknolojia unapaswa kuanzia katika kutambua changamoto halisi zinazohitaji kutatuliwa, badala ya kuingiza teknolojia bila kuelewa mahitaji ya watumiaji na mazingira husika.

Ameeleza kuwa katika programu ya miezi mitatu iliyohusisha vijana, mwezi wa kwanza ulitumika kubaini mahitaji kabla ya kuanza mafunzo ya teknolojia mwezi Agosti, ambapo Google pia ilialikwa kushiriki, na baadaye wanafunzi kuunda suluhisho bunifu zilizowasilishwa na timu tano mwezi Septemba.
Amesema mafanikio ya ushirikiano huo hayahitaji mifumo tata, bali kuwaunganisha wadau sahihi, kuwa na jukwaa la ushirikiano na kuweka taratibu madhubuti za utekelezaji, akisisitiza kuwa Tanzania ina rasilimali kubwa ya vijana wenye vipaji na uwezo wa kuzalisha suluhisho za changamoto mbalimbali.



