FSCs zageuka daraja la wakulima

IRINGA: WAKULIMA katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya wanaanza kupata huduma muhimu za kilimo karibu na maeneo yao kupitia Vituo vya Huduma kwa Wakulima (Farmer Service Centres—FSCs), vinavyolenga kubadilisha uzalishaji wa mazao kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo-biashara chenye tija.

Vituo hivyo vinajengwa kuwa kiungo kati ya mkulima na huduma muhimu katika mnyororo wa thamani, ikiwemo pembejeo bora, teknolojia, zana na mitambo ya kilimo, ushauri wa kitaalamu, taarifa za masoko, huduma za baada ya mavuno, wanunuzi na taasisi za fedha.

Hatua hiyo imekuja sambamba na makabidhiano ya vifaa vya kilimo vyenye thamani ya Sh Milioni 51.3, vilivyotolewa kwa ajili ya kuimarisha huduma katika vituo hivyo vinavyotekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.

Akizungumza katika mahafali ya waendeshaji wa FSCs mkoani Iringa, Mkurugenzi Mtendaji wa Nafaka Kilimo, Idd Kindamba, alisema lengo ni kujenga mfumo imara wa kilimo-biashara unaowawezesha wakulima kupata huduma muhimu karibu na maeneo yao na kuongeza tija, kipato na fursa za masoko.

Alisema FSCs zinatoa huduma mbalimbali ikiwemo pembejeo, zana na mitambo ya kilimo, ushauri wa kitaalamu, taarifa za masoko na huduma za baada ya mavuno, huku zikiwaunganisha wakulima na wanunuzi pamoja na taasisi za fedha.

“Lazima kuwe na uhakika wa mazao ambayo yanafikia soko na wakulima wapate soko linalofaa kwa mazao yao,” alisema Kindamba, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha uzalishaji na soko.

Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Mahamud Mabuyu, alisema kuongeza uzalishaji pekee hakutoshi kuimarisha usalama wa chakula na kipato cha wakulima, bali ni muhimu pia kupunguza gharama, kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuhakikisha mazao yanapata masoko yenye uhakika.

Alisema kupitia programu ya Farm to Market Alliance (FtMA), WFP inashirikiana na Nafaka Kilimo kujenga mfumo unaowawezesha wakulima kupata huduma za pembejeo, mitambo, upimaji wa unyevu, ushauri wa kitaalamu, taarifa za masoko na huduma za baada ya mavuno.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Patrick Mongela, alisema Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo kupitia mipango mbalimbali ikiwemo Agenda 10/30, inayolenga kukuza sekta hiyo kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030.

Alisema Serikali pia inaendelea kutekeleza Agriculture Master Plan 2050 na programu ya Building Better Tomorrow (BBT), zinazolenga kujenga sekta ya kilimo ya kisasa, shindani na inayotumia teknolojia na ubunifu katika uzalishaji na biashara.

Mongela alisema FSCs ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mipango hiyo kwa kuwa zinapeleka huduma karibu na wakulima na kuwaunganisha na pembejeo, teknolojia, zana, mitambo, masoko, taasisi za fedha na taarifa za biashara.

Katika hafla hiyo, Serikali na WFP zilikabidhi vipima unyevu wa mazao 15, mizani ya kidijitali 15 na maturubai 50, vifaa ambavyo vinatarajiwa kusaidia kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuboresha ubora wa mazao yanayopelekwa sokoni.

Mongela aliwataka waendeshaji wa FSCs kutumia na kutunza vifaa hivyo kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora, kuendesha vituo kwa uwazi na kujenga uaminifu kwa wakulima.

Aidha, alizitaka Halmashauri na serikali za mitaa kutambua FSCs kama wadau muhimu wa maendeleo ya kilimo na kushirikiana navyo katika utoaji wa huduma, huku sekta binafsi ikihimizwa kujenga mahusiano ya muda mrefu na wakulima kupitia vituo hivyo.

Alisema mafanikio ya FSCs yatapimwa kupitia ubora wa huduma zinazotolewa, uwezo wa vituo kujiendesha kifedha na mchango wake katika kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao, masoko na kipato cha wakulima.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button