‘Akili unde itaongeza ufanisi haichukui nafasi ya wafanyakazi’

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom imesema matumizi ya teknolojia ya akili unde yanalenga kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja na si kuchukua nafasi ya wafanyakazi.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom, Harriet Lwakatare, alisema hayo juzi wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wafanyakazi wa huduma kwa wateja iliyofanyika kuhitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Alisema pamoja na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo akili unde, mifumo ya kiotomatiki na roboti bado kuna changamoto zinazohitaji usikivu uwezo wa kibinadamu katika kufanya maamuzi na kuelewa mahitaji ya wateja.

“Teknolojia inaweza kuwepo, lakini mwanadamu bado tunamhitaji. Teknolojia inatusaidia kurahisisha kazi zinazojirudia, lakini kuna maswali na changamoto zinazohitaji mtu kusikiliza kwa kina, kuonyesha huruma na kuchanganua mambo ambayo mashine haiwezi kufanya,” alisema Lwakatare.

Alisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kuwawezesha wafanyakazi kutoa huduma bora zaidi kwa muda mfupi badala ya kuondoa nafasi zao za kazi.

Lwakatare alisema hafla hiyo ilikuwa sehemu ya kutambua mchango wa wafanyakazi wanaohudumia wateja kupitia vituo vya kupokea simu, maduka, vitengo vya nyuma vinavyoshughulikia changamoto za wateja na maeneo mengine ya kampuni hiyo.

Alisema kuwatambua wafanyakazi hao ni muhimu kwa kuwa kazi zao zina mchango katika utendaji, ukuaji na mafanikio ya kampuni.

“Sherehe kama hizi zinawakumbusha wafanyakazi kuwa wana thamani katika Vodacom Tanzania. Wanapoamka kesho kwenda kazini, wanakuwa na motisha zaidi ya kuendelea kutoa huduma bora,” alisema.

Meneja wa Maduka ya Rejareja wa kampuni hiyo,Vanessa Mlawi alisema wafanyakazi wa huduma kwa wateja ni kiungo muhimu kati ya kampuni hiyo kwa kuwa ndio wanaopokea na kushughulikia mahitaji yao ya kila siku.

Alisema kampuni hiyo inatambua mchango wa teknolojia katika kuboresha utendaji, lakini matumizi yake hayaondoi umuhimu wa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wafanyakazi na wateja.

Alisema kampuni hiyo pia ilishiriki kuchangiaji damu na kutembelea shule zinazohudumia wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wake na jamii.

Mteja wa Vodacom, Padili James alisema amekuwa akitumia mtandao huo kwa takribani miaka 17 na kufurahishwa na huduma za intaneti zinazomsaidia katika shughuli zake za kutengeneza maudhui na biashara.

James alisema huduma ya intaneti ya nyumbani ni miongoni mwa huduma anazozifurahia kwa kuwa inatoa vifurushi mbalimbali vinavyoweza kutumiwa na wanafamilia na majirani.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button