Zanzibar kuibua vipaji vya sayansi ya anga

ZANZIBAR: Watoto na vijana wenye umri wa miaka saba hadi 24 wamepewa fursa ya kuonesha ubunifu wao katika sayansi ya anga kupitia shindano maalum linalolenga kuwajengea uelewa na msingi wa maarifa yatakayowawezesha kushiriki katika teknolojia ya anga za juu siku zijazo.

Shindano hilo limeandaliwa na Zanzibar Astronomy and Space Society (ZASS), likiwa sehemu ya juhudi za kuwahamasisha watoto na vijana kupenda sayansi, ubunifu na taaluma zinazohusiana na anga na teknolojia.

Kupitia shindano hilo, washiriki wanatakiwa kutengeneza vielelezo vya vitu na mifumo ya angani, ikiwemo sayari, mfumo wa jua, galaksi, satelaiti na roketi. Washindi watatu watapatikana katika kila kundi na kupata zawadi za fedha taslimu kuanzia Sh300,000 hadi Sh1 milioni.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa ZASS, Malik Juma, amesema lengo la shindano hilo si kutambua washindi pekee, bali kuwajengea watoto na vijana msingi wa maarifa ya sayansi na kuwavutia kuingia katika taaluma zinazohusiana na anga na teknolojia.

“Lengo moja ni kuwahamasisha wanafunzi na watoto kupenda sayansi, lakini pia kuwaonesha mambo ya sayansi kupitia elimu ya masuala ya anga na anga za juu,” amesema Juma.

Amesema shindano hilo limegawanywa katika makundi matatu kulingana na umri, ambapo kundi la junior linahusisha watoto wenye miaka saba hadi 13, senior miaka 14 hadi 18 na advance miaka 19 hadi 24.

Kwa mujibu wa Juma, washiriki wanapaswa kuwasilisha kazi zao kuanzia Oktoba 12 hadi Oktoba 18, 2026, kwa njia ya video kupitia mitandao ya kijamii au kwa kuzipeleka moja kwa moja katika ofisi za ZASS zilizopo Tunguu-Kibele, Zanzibar.

Amesema kazi zitakazowasilishwa zinapaswa kuonesha uelewa wa washiriki kuhusu vitu na mifumo ya angani, huku kiwango cha ugumu kikizingatia umri na uwezo wa mshiriki.

Kwa watoto wadogo, amesema vifaa rahisi kama maboksi na karatasi vinaweza kutumika katika kutengeneza vielelezo, wakati vijana wakubwa wanatarajiwa kuwasilisha kazi zenye maelezo, ubunifu na kiwango cha juu zaidi cha uelewa.

Washiriki wanaweza kushindana mmoja mmoja au kwa vikundi, huku washindi watatu wakitarajiwa kupatikana katika kila kundi.

Shindano hilo linatarajiwa kuongeza hamasa kwa watoto na vijana kujifunza sayansi kwa njia ya vitendo, huku likiwapa nafasi ya kutumia ubunifu wao katika kuelewa teknolojia na mifumo ya anga.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button