Afrika yahimizwa kutumia AI kukuza uchumi

DAR ES SALAAM: Matumizi ya Akili Unde (AI), uwekezaji wa Waafrika ndani na nje ya bara pamoja na kuongeza thamani ya mazao, yameelezwa kuwa fursa muhimu zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha maendeleo ya Afrika.
Katika mkutano wa World CEO Summit Africa 2026 uliofanyika Dar es Salaam, washiriki walisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia teknolojia mpya, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kujenga uwezo wa wawekezaji wa ndani ili kunufaika zaidi na rasilimali zilizopo.
Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, amesema teknolojia ya Akili Unde (AI) inakua kwa kasi, hivyo kuzipa nchi za Afrika fursa ya kuruka baadhi ya hatua za maendeleo ambazo nchi zilizoendelea zilipitia.
Akitolea mfano Mauritius, amesema nchi hiyo imeanzisha kitengo cha AI chini ya Wizara ya Habari, hatua ambayo inaweza kuwa somo kwa Tanzania katika kuandaa mikakati ya matumizi ya teknolojia hiyo.
Juneid amesema pia kuna wazo la kuanzisha Chuo Kikuu cha AI nchini Tanzania, huku mazungumzo yakiendelea na mamlaka za Mauritius kuhusu uwezekano wa ushirikiano katika eneo hilo.
Amesema teknolojia hiyo ina fursa katika sekta mbalimbali, hivyo Afrika inapaswa kuwekeza katika maarifa na miundombinu ili kunufaika na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.
Katika eneo la uwekezaji, Juneid amesema Watanzania wana uwezo wa kuwekeza nje ya nchi kwa kufuata taratibu za kisheria, akitolea mfano uwekezaji katika majengo, ikiwemo Dubai.
Amesema changamoto kubwa inayokabili baadhi ya wawekezaji ni uelewa mdogo kuhusu fursa zilizopo na taratibu za kufanya uwekezaji wa kimataifa, ikiwemo namna ya kutuma fedha kupitia njia rasmi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na mwanzilishi wa Dejat Consult na GJB Group, CPA Dunstan Rushekya, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya biashara, urafiki na ushirikiano kati ya viongozi na wawekezaji wa Afrika.
Amesema mawasilisho kutoka Mauritius na Ghana yameonesha umuhimu wa kuunganisha fursa za kiteknolojia na kiuchumi, huku akisisitiza kuwa Afrika inahitaji kuondoa vikwazo vinavyozuia biashara na uwekezaji baina ya nchi zake.
Rushekya ametaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha uwekezaji kuwa ni uhitaji wa mtaji mkubwa, ukosefu wa taarifa kuhusu fursa zilizopo pamoja na vikwazo vya kisheria na kiuchumi vinavyotofautiana kati ya nchi.
Naye Dk. Jesca Nkwabi amesema Afrika ina soko kubwa kutokana na idadi ya watu na utajiri wa malighafi, lakini bado kuna nafasi ya kuongeza manufaa ya kiuchumi kupitia uchakataji wa bidhaa.
Dk. Nkwabi, ambaye amesema kampuni yake ina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika uchakataji wa mazao, uzalishaji viwandani na biashara, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya malighafi badala ya kuuza mazao ghafi nje ya nchi.
Ametolea mfano wa pamba, ambayo inaweza kuchakatwa na kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo pamba safi, mafuta ya kula kutoka kwenye mbegu zake na mashudu yanayotumika katika chakula cha mifugo.
Aidha, amesema uchakataji wa mchele unaweza kuwezesha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na kuifanya kampuni kujenga chapa zinazokidhi mahitaji ya soko.
Washiriki hao wameeleza kuwa kuunganisha teknolojia, uwekezaji na uzalishaji unaoongeza thamani ya malighafi kunaweza kusaidia Afrika kutumia rasilimali zake kwa tija, kupanua biashara na kuongeza nafasi za ajira.



