‘Shule zisizo na vifaa zisipokee wanafunzi wa amali’

MOROGORO: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewaagiza maofisa uthibiti ubora wa shule kufuatilia shule zote zinazotoa elimu ya amali na kuhakikisha zina miundombinu, vifaa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi.
Amesema shule zilizosajiliwa kutoa elimu ya amali lakini hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia hazipaswi kuendelea kupokea wanafunzi wa mkondo huo hadi zitakapokamilisha mahitaji yanayohitajika.

Profesa Mkenda ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya maofisa uthibiti ubora wa shule kuhusu timu za uthibiti ubora wa shule za ndani, yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Morogoro.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Uongozi imara wa timu za uthibiti ubora wa shule za ndani ni msingi wa elimu bora na ujenzi wa umahiri.”
Amesema kukosekana kwa vifaa katika shule zinazotambulika kuwa za amali kunaweza kusababisha jamii kupoteza imani na mfumo huo, licha ya umuhimu wake katika kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo.

“Wazazi wengi wanavutiwa na mfumo huo kwa kuwa wanafunzi wanapohitimu hupata vyeti vya elimu ya sekondari pamoja na sifa za ufundi, jambo linalowawezesha kuendelea na kidato cha tano au vyuo vya ufundi,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amewaagiza maofisa uthibiti ubora pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule kupitia shule zote zilizopokea wanafunzi wa mkondo wa amali na kubaini kama zina vifaa vinavyohitajika.
Amesisitiza kuwa shule ambazo hazijakidhi vigezo hivyo zinapaswa kupokea wanafunzi wa mkondo wa elimu ya jumla badala ya amali hadi zitakapokuwa tayari kutoa mafunzo hayo.

Amesema bila vifaa vinavyohitajika, wanafunzi watakosa maandalizi ya kutosha kwa mitihani ya vitendo, ikiwemo mitihani ya kidato cha pili, hivyo kuwataka maofisa hao kutoa taarifa kwake kuhusu shule zitakazobainika kuwa na changamoto hizo.
“Ni muhimu shule za sekondari za mkondo wa amali zijengwe kwa ukamilifu wake na ziwe na utoshelevu wa vifaa na vitendea kazi ili kukidhi matarajio ya kuanzishwa kwake,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amewataka maofisa uthibiti ubora kufuatilia kwa karibu ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu ya shule, ikiwemo madarasa na vyoo, akisema wanafunzi hawawezi kupangiwa shule ambazo hazijakamilisha mahitaji muhimu.
Ametoa mfano wa shule iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kubakiwa na kazi ndogo kama ujenzi wa vyoo, akisema maofisa hao wanapaswa kuishauri halmashauri na mkurugenzi kutenga fedha za kukamilisha ujenzi huo ili shule iweze kufunguliwa.
Amesema maofisa hao wanaweza pia kutoa elimu kwa madiwani kuhusu umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa na vyoo, hatua itakayochochea wananchi kuendelea kushiriki katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Aidha, amewataka kuhakikisha ushauri na usimamizi wanaoutoa unazingatia vigezo na viwango vinavyotakiwa katika ujenzi na uendeshaji wa shule.




NEW88 – Sân chơi giải trí hàng đầu với nhiều chương trình khuyến mãi hấp dẫn tham gia tại website: https://loinaithefof.ru.com/