Tanzania yatetea kiti baraza la uongozi ITU

Matokeo ya uchanguzi huo uliofanyika Doha, Qatar yanaiwezesha Tanzania kuendelea kushiriki katika uongozi

Doha, Qatar: TANZANIA imechaguliwa tena kuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Uongozi la Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) kwa kundi la Afrika kwa kipindi cha mwaka 2027–2030, baada ya kupata kura 131.

Hatua hiyo inaipa taifa hili kutoka ukanda wa Africa Mashariki nafasi kuendeleza juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa intaneti kwa gharama nafuu na kuongeza nafasi ya nchi zinazoendelea katika uchumi wa kidijitali.

Matokeo ya uchanguzi huo uliofanyika Doha, Qatar yanaiwezesha Tanzania kuendelea kushiriki katika uongozi wa taasisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya mawasiliano ya simu.

Pia yanaipa Tanzania jukwaa la kuendeleza suala muhimu katika sera yake ya kidijitali, ambalo ni kuhakikisha kuwa uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano unazalisha huduma ambazo wananchi wanaweza kuzimudu kifedha na kuzitumia.

Akizungumza wakati wa mkutano huo unaoendelea hadi Novemba 27, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Angellah Kairuki, amesisitiza uhusiano uliopo kati ya miundombinu ya mawasiliano na ushirikishwaji wa wananchi.

SOMA: Uzinduzi wa minara 758, maunganisho ya mkongo wa mawasiliano

Mpango wa Tanzania wa kuunganisha maeneo ya vijijini na huduma za mawasiliano unatoa mfano halisi wa uwekezaji unaofanyika katika kutekeleza ajenda hiyo na taarifa mradi zilizochapishwa na ITU ikisifu hatua ya Serikali ya Tanzania ya kujenga minara 758 ya mawasiliano katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, na kunufaisha takribani vijiji 1,400 pamoja na watu zaidi ya milioni 8.5.

Tanzania pia imehusisha ushirikishwaji wa kidijitali na usimamizi wa teknolojia zinazoibukia ambapo katika tamko la kisera, Waziri Kairuki alihimiza masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi na usalama wa mtandaoni kujumuishwa katika miundombinu ya kidijitali ya umma na kuongeza ushiriki wa nchi zinazoendelea katika kuunda sera na mwelekeo wa teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence – AI).

Vipaumbele hivyo vinaunganisha upanuzi wa upatikanaji wa huduma za kidijitali na mazingira yanayohitajika ili kujenga na kudumisha imani ya wananchi katika mifumo hiyo.

Aidha, Kairuki alielezea utayari wa Tanzania kushirikisha mataifa mengine mfano wa mfumo wake wa Klabu za Kidijitali (Digital Clubs), pamoja na kushirikiana na ITU na wadau wake katika kuendeleza ujuzi wa kidijitali na teknolojia ya akili unde katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kupata muhula mwingine katika Baraza hilo kunaipa Tanzania fursa ya kuendeleza ushirikiano huo na kuwasilisha uzoefu wake katika kuunganisha maeneo ya vijijini na huduma za mawasiliano ili uwe sehemu ya shughuli na mipango ya taasisi hiyo

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button