Bil 37.55/- kupeleka maji Misungwi, Kwimba

MWANZA: Zaidi ya wananchi 85,468 katika Halmashauri za Wilaya za Misungwi na Kwimba mkoani Mwanza wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji unaotekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 37.55, kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.
Mradi huo wa kusambaza maji kupitia mabomba kutoka Ukiliguru, Kolomije na Usagara hadi vijiji vya Sumve unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali.
Akizungumza leo Oktoba 13, 2026 alipotembelea mradi huo wilayani Misungwi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.
Amesema mradi huo unatarajiwa kusambaza maji katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Koromije na Bugomba, kupitia mtandao wa mabomba wenye urefu wa takribani kilomita 275.

Ameeleza kuwa mradi huo utasaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa maji inayowakabili wananchi, hususan wanawake ambao hutumia muda mwingi kutafuta maji visimani au kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Makonda amesisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi huo ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Godfrey Sanga, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Februari 21, 2023, na unatarajiwa kukamilika Desemba 17, 2027.
Amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Emirates Builders Limited chini ya usimamizi wa RUWASA, kwa gharama ya Sh bilioni 37.55 zinazofadhiliwa na Serikali.



