Makonda aipongeza TPA, atoa msisitizo Bandari Mwanza

MWANZA: WAZIRI wa Habari, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapaswa kuhakikisha mradi wa ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini unakamilika kwa wakati ili kuimarisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo.

Makonda amesema hayo leo alipofanya ziara mkoani Mwanza na kutembelea bandari hiyo, ambapo amesisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi huo kwa wakati. Pia, ameipongeza TPA kwa kazi inayofanya kuboresha miundombinu ya bandari na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha bandari kuhudumia meli tano kwa wakati mmoja, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji kupitia Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Rosemary Ndesamburo, amesema Serikali kupitia TPA inaendelea kutekeleza miradi ya upanuzi na uboreshaji wa bandari za Ziwa Victoria kwa awamu, kwa lengo la kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya biashara na usafirishaji.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo ulianza baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu mwaka 2022, uliosaidia kubainisha mahitaji ya bandari hizo, mbinu bora za kuziboresha na maeneo ya kupewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Ndesamburo, maboresho yalianza katika Bandari ya Mwanza Kaskazini, Bukoba na Kemondo, ambapo miradi hiyo inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali.

Amesema miradi hiyo imeanzishwa kutokana na ongezeko la watu, ukuaji wa biashara na mahitaji makubwa ya huduma za usafirishaji. Ameeleza kuwa Serikali inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha bidhaa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi nyingine kupitia Ziwa Victoria.

Aidha, amesema maboresho hayo yanatarajiwa kusaidia kukabiliana na ongezeko la shehena litakaloweza kusababishwa na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama wa bandari.

Amesema mradi wa ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 18.61, kiasi kinachojumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Ameongeza kuwa mkataba wa usimamizi wa ujenzi una thamani ya Dola za Marekani milioni 1.58, bila kujumuisha VAT inayohusika kwa mujibu wa mkataba.

Amesema hadi Oktoba 2026, mkandarasi alikuwa amelipwa Sh bilioni 10.84 kupitia hati tisa za malipo, huku hati ya kumi yenye thamani ya Sh bilioni 1.04 ikiwa katika hatua za mwisho za malipo.

Ameeleza kuwa mradi huo umechangia kutoa ajira za muda kwa wananchi 300 na kuongeza fursa za biashara kwa wajasiriamali wadogo wanaotoa huduma za chakula, malazi na usafiri.

Vilevile, amesema shughuli za ujenzi zinachangia mapato ya Halmashauri kupitia kodi, ushuru na tozo mbalimbali. Ameongeza kuwa mradi huo unawapa vijana wa Kitanzania nafasi ya kupata ujuzi na uzoefu katika sekta ya ujenzi na usanifu.

Amesema baada ya kukamilika, bandari hiyo inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia meli tano kwa wakati mmoja, huku jengo jipya la kisasa litakalojengwa likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 700 kwa wakati mmoja.

Ameeleza kuwa uboreshaji huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za bandari, kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kukuza biashara na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani zinazounganishwa na Ziwa Victoria.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button