Michezo ya 19 ya bandari yafunguliwa Moro

MOROGORO; WANAMICHEZO 466 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Bandari za Maziwa na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), wanashiriki Michezo ya 19 ya Bandari inayofanyika mjini Morogoro.
Michezo hiyo imefunguliwa leo na itafanyika kwa siku nne hadi Oktoba 15, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri na viwanja vya Bwalo la Umwema, Morogoro.
Akifungua michezo hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi, tija na ushindani katika sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo sekta ya bandari inayotajwa kuwa lango muhimu la biashara na uchumi wa Taifa.

Amesema michezo ina mchango mkubwa katika kujenga afya ya mwili na akili, nidhamu, uvumilivu, ushirikiano na uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja.
Kilakala amesema umuhimu wa watumishi wa sekta ya bandari kuwa na afya bora ni mkubwa kutokana na aina ya shughuli wanazozifanya, ambazo zinahitaji umakini, uwajibikaji, weledi na utayari wa kutoa huduma wakati wote.
Amesema michezo hiyo inapaswa kuwa sehemu ya juhudi za taasisi katika kujenga mazingira bora ya kazi na kuimarisha mahusiano miongoni mwa wafanyakazi.

Mkuu huyo wa Wilaya amewapongeza viongozi wa TPA na taasisi zinazoshiriki kwa kuendelea kuandaa michezo hiyo kila mwaka, akisema kufanyika kwake kwa mara ya 19 ni ishara ya nafasi yake katika kujenga utamaduni wa michezo na ustawi wa wafanyakazi.
“Kuendelea kwa michezo hii kwa mara ya 19 ni ishara kwamba imekuwa na nafasi muhimu katika kujenga utamaduni wa michezo na ustawi wa wafanyakazi,” amesema Kilakala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema michezo ya mwaka huu inashirikisha wanamichezo kutoka vituo mbalimbali vya bandari nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano mema kazini.

Amesema michezo hiyo inafanyika chini ya kaulimbiu: “Michezo ya Bandari 2026: Michezo ni chanzo cha furaha, afya bora na ubunifu endelevu kwa maendeleo ya bandari na Taifa kwa ujumla.”
Mbossa amesema wanamichezo hao wanashindana katika michezo mbalimbali, ikiwemo soka, mpira wa kikapu, netiboli, mpira wa wavu, kuvuta kamba na riadha.
Amesema pia michezo hiyo inahusisha michezo ya jadi kama bao, karata na drafti, ambayo inatoa fursa kwa watumishi kushiriki katika shughuli za kimichezo na kujenga mshikamano.
“Lengo letu si kushindana pekee, bali pia kuimarisha afya, mshikamano, nidhamu na mahusiano mema miongoni mwa wafanyakazi,” amesema Mbossa.

Amesema TPA itaendelea kuendeleza utamaduni wa michezo kwa lengo la kuchangia ustawi wa watumishi na kuongeza ufanisi katika sekta ya bandari.



