Kombe la EPL latua Tanzania

DAR ES SALAAM: KOMBE la Ligi Kuu ya England limewasili Tanzania kwa mara ya kwanza, likianza ziara yake ya Afrika Mashariki kupitia udhamini wa kampuni ya bia ya Guinness, ambayo ni mmoja wa wadhamini wa vinywaji wa ligi hiyo.

Kuwasili kwa kombe hilo Oktoba 9, 2026, kumeashiria kuanza kwa shughuli za siku mbili zinazolenga kuwaunganisha mashabiki wa soka nchini na moja ya mashindano yanayofuatiliwa kwa karibu duniani.

Kupitia ziara hiyo, Guinness inalenga kuunganisha umaarufu wa soka la kimataifa na utamaduni wa soka nchini, ambako mashabiki wamekuwa wakifuatilia ligi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia ujio huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries, Dk. Obinna Anyalebechi, amesema Ligi Kuu ya England ina nafasi kubwa katika mioyo ya mashabiki wengi wa soka nchini, hivyo kuwasili kwa kombe hilo kunawapa fursa ya kukutana na alama muhimu ya mashindano hayo.

Amesema lengo ni kuandaa tukio linaloonyesha utamaduni wa Tanzania na kuunganisha soka la kimataifa na nguvu, ubunifu na mapenzi ya Watanzania kwa mchezo huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries, Henry Esiaba, amesema Tanzania ina utamaduni mkubwa wa soka na ujio wa kombe hilo ni fursa ya kushuhudia kwa karibu hamasa ya mashabiki.

Amesema kampuni hiyo inalenga kuhakikisha tukio hilo linaakisi uhalisia wa soka la Tanzania kwa kuwapa mashabiki nafasi ya kushiriki, kusimulia uzoefu wao na kusherehekea mchezo huo.

Ujio wa kombe hilo pia umehusishwa na utamaduni wa ushindani wa soka nchini, hususan kupitia mashabiki wa klabu za Simba SC na Young Africans (Yanga), ambazo zina wafuasi wengi na ambao pia hufuatilia Ligi Kuu ya England.

Akizungumza kwa niaba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Aaron Nyanda amesema kuwasili kwa kombe hilo kunaonyesha uhusiano uliopo kati ya jamii ya soka nchini na mashindano ya kimataifa.

Amesema mashabiki wa Tanzania hufuatilia soka katika ngazi mbalimbali, kuanzia klabu za ndani hadi ligi na mashindano ya kimataifa, hivyo tukio hilo linawapa nafasi ya kukutana na soka la kimataifa kwa namna tofauti.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema michezo ina nafasi muhimu katika kuwaunganisha watu, kutengeneza fursa kwa vijana na kuipa nchi nafasi ya kuonyesha utamaduni na utambulisho wake.

Amesema kuwasili kwa kombe hilo si tukio kwa mashabiki wa soka pekee, bali pia ni fursa ya kuonyesha nafasi ya michezo katika jamii ya Tanzania.

Baada ya ziara yake nchini Tanzania, kombe hilo linatarajiwa kuendelea na safari yake nchini Uganda kuanzia Oktoba 11 hadi 13, kabla ya kuelekea Kenya.

Kuhusu Ligi Kuu ya England

Ligi Kuu ya England ni miongoni mwa mashindano ya soka yanayofuatiliwa na mashabiki wengi duniani. Kupitia ligi hiyo na klabu zinazoshiriki, mashabiki kutoka mataifa na tamaduni mbalimbali huunganishwa na mchezo wa soka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kuhusu ligi hiyo, mashindano hayo yanafikia watazamaji katika kaya milioni 920 katika nchi 189 duniani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button