Vijana vijiji 11 kupata fursa kuonesha vipaji

MARA: VIJANA kutoka vijiji 11 vinavyozunguka Mgodi wa Barrick North Mara wanatarajiwa kupata fursa ya kuendeleza vipaji vyao na kutumia michezo kama njia ya kujiajiri na kujipatia kipato kupitia mashindano ya Mahusiano Cup yaliyozinduliwa na mgodi huo.

Mashindano hayo yanalenga kuwapa vijana jukwaa la kuonyesha uwezo wao katika michezo mbalimbali, huku yakifungua fursa za kutambua na kuendeleza vipaji vinavyoweza kuwa chanzo cha ajira na kipato.

Meneja wa Mgodi wa North Mara, Stephen Doyle, amesema uwekezaji katika michezo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za mgodi katika kuchangia maendeleo ya jamii na kuimarisha ushirikiano na wananchi wanaozunguka mgodi.

 

Amesema michezo ina nafasi muhimu si tu katika kukuza vipaji, bali pia kuimarisha afya, kujenga mshikamano na kuleta ustawi wa jamii.

Ameongeza kuwa Baraza la Maendeleo ya Jamii (CDC) liliwasilisha ombi kwa mgodi kusaidia maendeleo ya michezo, hususan mpira wa miguu.

Amesema eneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja tayari limepatikana, lakini utekelezaji wa mradi huo unasubiri kukamilika kwa taratibu za upatikanaji wa hati ya eneo hilo.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa kampuni ya mgodi wa Barrick, Francis Uwadi, amesema mashindano hayo yametokana na kutambua nafasi ya michezo katika kuimarisha mahusiano kati ya mgodi na jamii.

Amesema Mahusiano Cup litafanyika kwa wiki nzima, likihusisha michezo mbalimbali, huku vijiji vitakavyofanya vizuri vikipatiwa zawadi kwa lengo la kuongeza hamasa na kuendeleza vipaji vya vijana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button