TPA yabeba medali tisa riadha Moro

MOROGORO: TIMU ya riadha ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imehitimisha kwa mafanikio katika mchezo wa riadha kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) 2026, yanayoendelea mkoani Morogoro kwa kutwaa jumla ya medali tisa.
Katika mashindano hayo, TPA imefanikiwa kujinyakulia medali tatu za dhahabu, tatu za fedha na tatu za shaba, matokeo yanayoonesha kuimarika kwa kiwango cha wanariadha wa Mamlaka hiyo ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Akizungumza kufuatia kuhitimishwa kwa mchezo huo, Meneja wa Mchezo huo wa TPA, Leslie Omary, amesema mafanikio hayo ni ishara ya maendeleo ya mchezo wa riadha ndani ya TPA.
“ Matokeo ya mwaka huu yameonesha ya kwamba tumepiga hatua kubwa ikilinganishwa na ushiriki wa miaka iliyopita” amesema Omary
Menej awa Mchezo huo amesema, TPA imehitimisha safari yake ya riadha katika SHIMMUTA 2026 kwa mafanikio makubwa, ikionesha ushindani, juhudi na mshikamano wa wanamichezo wake.

Katika mchezo huo, Shagi Luguwa alishinda mbio za mita 200 kwa wanaume ya kunyakua medali za dhahabu, huku timu ya TPA ya kupokezana vijiti mita 4×100 kwa wanaume, iliyoundwa na Shagi Luguwa, Elias, Ramadhani na Aziz, nayo ikiibuka mshindi wa nafasi ya kwanza na kutwaa medali za dhahabu.
Mchezaji mwingine Joseph Mwambipile alishinda medali ya dhahabu katika mashindano ya kurusha tufe.
Kwa upande wa Medali za fedha zimepatikana kupitia mchezaji Naomi Chambo, aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za mita 100 na 200 kwa wanawake, pamoja na Ramadhani Masoud aliyeshika nafasi ya pili katika mchezo wa kukimbia na magunia.

Katika medali za shaba, pia Naomi Chambo, Suzy, Fatuma na Elieth ameipatia TPA medali hizo kwenye mbio za kupokezana vijiti mita 4×100 kwa wanawake.
Medali nyingine zimepatikana kupitia Azizi Ally kwa mbio za mita 100 kwa wanaume na Hinju Damas katika mita 400 kwa wanaume.



