TPA yatinga mtoano SHIMMUTA, yaendelea kutamba netiboli, kamba

MOROGORO: TIMU za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika michezo ya soka, netiboli na kuvuta kamba zimefuzu hatua ya mtoano katika mashindano ya SHIMMUTA yanayoendelea kutimua vumbi mjini Morogoro.

Katika mchezo wa Soka, TPA imehitimisha hatua ya makundi ikiwa nafasi ya pili katika Kundi C, kwa kujikusanyia jumla ya alama 10, nyuma ya TANESCO, na hivyo kujihakikishia tiketi ya kusonga mbele katika hatua ya 32 bora.
Kwa upande wa Netiboli, TPA, ambayo ni bingwa mtetezi, imeendelea kuonyesha ubora wake kwa kusonga mbele na kuimarisha matumaini ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya sita mfululizo, ikiwa na dhamira ya kuendeleza rekodi yake ya kutawala mchezo huo.

Nayo timu ya Kuvutana kwa Kamba kwa upande wa wanaume na wanawake imefanikiwa kusonga mbele katika hatua ya robo Fainali, ikiwa katika harakati za kutetea mataji yake. Timu hizo zimeendelea kuonyesha ubabe na uimara wao, huku wapinzani wakishindwa kuhimili nguvu ya wawakilishi hao wa TPA.

Matokeo hayo yanaendelea kudhihirisha maandalizi mazuri, nidhamu, mshikamano na ushindani wa hali ya juu unaoonyeshwa na wanamichezo wa TPA katika mashindano hayo, huku wakilenga kuendeleza mafanikio na kuipa heshima Mamlaka.



