EAC yataka posta za kidigitali kurahisisha biashara

ARUSHA: NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuimarisha mifumo ya kidijitali, miundombinu ya usafirishaji na ushirikiano wa kikanda ili kurahisisha biashara za mtandaoni na kuboresha upatikanaji wa huduma za posta kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Switbert Mkama, wakati akifungua Jukwaa la Tano la Posta na Usafirishaji Afrika Mashariki, lililofanyika Arusha.

Dk. Mkama amesema kukua kwa biashara za mtandaoni kunahitaji huduma bora za posta, mifumo ya malipo ya kidijitali inayopatikana kwa urahisi, gharama zilizo wazi pamoja na mifumo ya uhakika ya kufikisha bidhaa kwa wateja.

Amesema uimarishaji wa huduma hizo utasaidia wananchi na wafanyabiashara, wakiwemo waliopo vijijini na maeneo ambayo hayajafikiwa vya kutosha, kutumia fursa za biashara mtandaoni bila kukumbana na changamoto za upatikanaji wa huduma za usafirishaji.

Aidha, amezitaka nchi wanachama kuimarisha mifumo ya malipo na usafirishaji inayoweza kuwasiliana, kuoanisha viwango vya teknolojia na kuboresha mafunzo ya kitaaluma ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Dk. Peter Kihogo, amesema mfuko huo unaendelea kusaidia maboresho ya sekta ya posta nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, vifaa vya kidijitali na upanuzi wa huduma za posta vijijini.

Amesema hadi Juni 2026, mtandao wa mawasiliano ya simu wa kizazi cha nne (4G) ulikuwa umefikia asilimia 94 ya wananchi, hatua inayoweka msingi wa kuimarisha huduma za kidijitali na usafirishaji wa vifurushi.

Ameongeza kuwa UCSAF imesambaza vifaa vya kidijitali zaidi ya 500 kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa vifurushi na uingizaji wa taarifa za wateja katika mifumo ya posta.

Aidha, mfuko huo umetoa kompyuta 100 kwa ajili ya kuboresha shughuli za posta vijijini na mashine 50 za kunakili nyaraka zinazoshikiliwa kwa mkono kwa ajili ya kuboresha huduma katika madawati ya mapokezi.

Katika mwaka wa fedha 2026/2027, UCSAF imepanga kujenga majengo 31 ya posta vijijini, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema Mkoa wa Arusha umependekezwa kuwa eneo la majaribio la kuanzisha na kuimarisha huduma za posta za kidijitali nchini.

Amesema mpango huo unalenga kuzibadilisha ofisi za posta kuwa vituo vya kisasa vitakavyowaunganisha wananchi na wafanyabiashara na huduma za biashara mtandaoni, malipo ya kidijitali, huduma za serikali mtandao na mifumo ya kisasa ya usafirishaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button