Serikali: Taasisi ziwezeshe wanawake kiuongozi

DAR ES SALAAM; Serikali imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikisisitiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na uamuzi shirikishi unaotoa nafasi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha, imetaja mambo matano kwa viongozi wa taasisi, waajiri na wadau wa maendeleo kuyapa kipaumbele na kusimamia utekelezaji wake ili kuchochea uendelevu wa wanawake katika uongozi Tanzania.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Riziki Pembe, kuendeleza viongozi wanawake ni sehemu ya kujenga uongozi utakaosaidia kufikia malengo makubwa yaliyoj katika dira hiyo.

Wakati Dk Riziki akisema hivyo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray amesisitiza waajiri kutoa fursa kwa haki na usawa kwa kuzingatia sifa na vigezo huku wakiepuka ubaguzi wa kijinsia.

Ametaka viongozi wakiwamo wanawake kuandaa na kulea wanawake wengine ili wawe tayari kubeba vema majukumu ya uongozi, badala ya kuwakandamiza.

 


Naibu waziri huyo ametaka waajiri katika taasisi za umma kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya watumishi ili kuongeza ufanisi kazini, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji huduma.

Amesema mafunzo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa kufanya uamuzi unaojikita katika taarifa sahihi, kuimarisha ushirikiano, kutumia teknolojia na kusimamia rasilimali watu.

Mawaziri hao walikuwa wakizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Sita tangu kuzinduliwa kwa Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika Dar es Salaam chini ya kaulimbiu: ‘Kukuza Uendelevu wa Wanawake katika Uongozi Barani Afrika.’

Kwa mujibu wa Dk Riziki, dhamira hiyo inaungwa mkono na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.
“Shabaha ya 5.5 inasisitiza ushiriki kamili na wenye ufanisi wa wanawake na fursa sawa za uongozi katika ngazi zote za maamuzi,” amesema.

Akaongeza: “Shabaha za 5.1 na 5.2 zinalenga kuondoa ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, huku shabaha ya 5.c ikisisitiza kuandaa sera na sheria zinazotekelezeka kwa ajili ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.”

Riziki amesema shabaha hizo zinatoa msingi wa kujenga mazingira yanayowawezesha wanawake kushiriki na kuendelea kukua katika uongozi.

 

Kuhusu programu hiyo inayoandaliwa na Taasisi ya Uongozi Dk Riziki anasema: “Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake inachangia dhamira hii kwa kuwajengea washiriki maarifa na ujuzi wa kutekeleza majukumu yao na kujiandaa kwa nafasi za juu zaidi.”

Kwa Zanzibar, Waziri Riziki amesema: “Serikali imeweka usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ndani ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 ikilenga kujenga jamii yenye usawa, inayolinda haki za wanawake na kuwawezesha kupata fursa za kiuchumi, huduma na ajira zenye staha.”

Akaongeza: “Katika viashiria vyake, Dira inaweka shabaha ya uwakilishi wa wanawake katika nafasi husika za maamuzi katika sekta ya umma kufikia asilimia 40 mwaka 2030, asilimia 50 mwaka 2040 na kuendelea katika kiwango hicho mwaka 2050.”

Dk Riziki amesema viongozi wa taasisi wanapaswa kuhakikisha kuna uwazi na usawa katika uteuzi, tathmini ya utendaji na kupandishwa vyeo kati ya wanawake na wa wanaume.

“Wanawake wapewe fursa za kuongoza majukumu muhimu, kuonesha uwezo wao na kujiandaa kwa nafasi za juu zaidi na viongozi wasimamie utekelezaji wa taratibu za kuzuia na kushughulikia ubaguzi na unyanyasaji mahali pa kazi,” alisema.

Katika Kongamano lililokutanisha viongozi wa kisiasa, biashara, wasomi na wadau wa maendeleo kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika, Dk Riziki amesema taasisi hazina budi kuimarisha mifumo ya kuandaa na kujenga viongozi wanaochipukia.

“Viongozi wenye uzoefu, wanawake na wanaume, wasaidiwe kwa maarifa na kuwaunganisha na mitandao ya kitaaluma na fursa za maendeleo,” amesema.

Akaongeza: “Najua hata wanawake na wanaume wapo wengine ambao ni viongozi mizigo, sasa wale ambao ni wazuri hasa wanawake au, tuendelee kuwa nao ili taifa lifaidi utumishi wao.”

Aidha, ametaka Taasisi ya Uongozi kutumia mtandao wa wahitimu wa programu hiyo kuendeleza ushirikiano, kubadilishana uzoefu, maarifa na ushauri na kusaidiana katika kutatua changamoto za uongozi.

“Tatu, waajiri waweke mazingira yanayosaidia viongozi kutekeleza majukumu ya kazi na familia…. Kwa mfano, kama mama ananyonyesha kwanini umpange ‘shift’ (zamu) ya usiku, kujifungua na kunyonyesha hakuondoi haki zake,” amesema Dk Riziki.

Akaongeza: “Sambamba na hilo, tuhimize mgawanyo wa majukumu ya malezi nyumbani na ushiriki wa wanaume katika kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake… Ushirikiano huu uendelee katika taasisi zetu na uonekane katika fursa na msaada wanaopata viongozi wanawake.”

Ametaka Taasisi ya Uongozi kundeleza na kukamilisha utafiti kuhusu uendelevu wa wanawake katika uongozi kwa kuzingatia michango ya mawazo katika kongamano hilo na kuwasilisha mapendekezo kwa wadau wanaohusika.

“Taasisi zitumie ushahidi wa utafiti kuboresha mifumo yao na kuimarisha utendaji kazi. Katika kupima maendeleo, tuzingatie uwakilishi wa wanawake, fursa zao za kukua, muda wa kuhudumu na sababu zinazowafanya kuondoka katika nafasi za uongozi,” amesema.

Amehimiza wakuu wa taasisi za umma na binafsi kuendelea kusimamia masuala ya jinsia na kuandaa mpango wa kuwaendeleza viongozi wanawake.

“Katika mpango huo wabainishe wahusika, muda wa utekelezaji na viashiria vya kupima maendeleo. Utekelezaji ufuatiliwe na taarifa zitolewe kupitia taratibu za kawaida za taasisi,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button