‘NSSF ni fursa ya vijana kujikwamua kiuchumi’

RUKWA; Vijana nchini wametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na taasisi mbalimbali, ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kujikwamua kiuchumi na kujiandaa kwa maisha ya sasa na ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Suleiman Ameir, wakati akifunga Kongamano la Vijana lililofanyika katika Ukumbi wa Nazareth, wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na vijana zaidi ya 1,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana kuelekea kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mkoani Rukwa.

Amesema vijana wanapaswa kutafuta na kutumia fursa zilizopo, kuongeza ujuzi na kutumia vipaji na uwezo wao kujiajiri au kuajiriwa.

Alisisitiza pia umuhimu wa kuweka akiba na kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii ili kuwa na maandalizi mazuri ya kukabiliana na changamoto za maisha.

Alieleza kuwa vijana waliojiajiri na walioajiriwa wanapaswa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF na ZSSF, kupitia programu zinazowafaa, kama vile Hifadhi Skimu na Weka Tuweke, kwa kuzingatia masharti ya kila mpango.

Ametaka viongozi wa serikali, taasisi na wadau wengine kuhakikisha kuwa mazingira ya kiuchumi na kijamii yanawezesha vijana kupata fursa za kujikwamua na kutimiza malengo yao.

Kupitia Hifadhi Skimu, NSSF inatoa fursa kwa wananchi waliojiajiri, wakiwemo waendesha bodaboda, wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji wadogo wa madini, mama na baba lishe, wasanii na wajasiriamali wengine, kujiunga na mfumo wa hifadhi ya jamii na kupata mafao kwa mujibu wa masharti ya mpango huo.

Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Rukwa, Nsengiyuva Msechu, aliwahimiza vijana kujiunga na Hifadhi Skimu mapema na kufanya uchangiaji kuwa sehemu ya mipango yao ya kifedha, akieleza kuwa utaratibu huo unaweza kuwasaidia kuimarisha usalama wao wa kifedha wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.

Msechu alisema mwanachama anayechangia kiwango cha chini cha Sh 30,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo anaweza kupata mafao ya matibabu kwa ajili yake mwenyewe, huku anayechangia Sh 52,200 kwa mwezi akipata fursa ya kupata mafao hayo kwa ajili yake na familia yake, kwa kuzingatia masharti ya mpango husika.

Aliongeza kuwa NSSF imerahisisha taratibu za kujiunga na kuchangia kupitia mifumo ya kidijitali, ikiwemo simu za mkononi na njia mbalimbali za malipo ya kifedha, ili kuwawezesha wanachama kuchagua njia inayowafaa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wao, baadhi ya vijana walioshiriki kongamano hilo waliishukuru NSSF kwa kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, wakieleza kuwa elimu hiyo imewasaidia kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii na kupanga maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button