SACCOS zatakiwa kutoa mikopo yenye tija

DAR ES SALAAM: Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vimetakiwa kuhakikisha mikopo inayotolewa inawawezesha wanachama kukuza biashara, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT 1992 LTD), Hassan Mnyone, amesema SACCOS zinapaswa kutoa huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wanachama na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Collins Nyakunga, amesema Tanzania imepata fursa ya kuandaa kongamano la kimataifa kutokana na mafanikio katika usimamizi na uendelezaji wa vyama vya ushirika.

Amesema kongamano hilo litajadili namna ya kuhakikisha wanachama wananufaika na mikopo na kuhamasisha watu wengi zaidi kujiunga na SACCOS.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika Tanzania, Godfrey Ng’urah, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na SACCOS kwa kutoa huduma zitakazosaidia kuongeza mitaji na kupanua shughuli za kiuchumi.

Wazungumzaji hao wameeleza hayo kuelekea na wakati wa Kongamano la Vyama vya Akiba na Mikopo Afrika (SACCA Congress 2026), lililowakutanisha wadau zaidi ya 600 kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

Kongamano hilo limeanza Oktoba 11 na litafungwa rasmi Oktoba16,mwaka huu.
Mwisho

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button