Mkuranga yaagizwa kukamilisha shule ya ufundi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kuhakikisha ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ufundi ya Mkuranga unakamilika mapema ili wanafunzi waanze kusoma ifikapo Januari 2027.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alitoa maagizo hayo jana wakati akikagua ujenzi wa shule hiyo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.6 iliyopo kata ya Mkamba wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.

Pia aliutaka uongozi wa Halmashauri kufuata taratibu zote za kisheria ili kutimiza ombi la wananchi ambao waliomba shule hiyo ipewe jina la Mbunge wa Jimbo la Mkuranga na Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega.

Awali alisema uwekezaji wa majengo ya shule hiyo utakuwa na tija pale yatakapoanza kutumiwa na wanafunzi kupata elimu na ujuzi wa ufundi.



