Mbegu bora suluhisho kukabili mabadiliko tabianchi

TANGA: WAKALA wa Mbegu za Kilimo (ASA) umehamasisha wakulima kutumia mbegu bora zinazolingana na mazingira yao na zinazoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kuongeza tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Elimu hiyo imetolewa katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika mkoani Tanga, ambapo wananchi waliotembelea banda la ASA wamepata fursa ya kujifunza aina mbalimbali za mbegu bora, sifa zake, maeneo yanayofaa kwa kilimo chake na namna sahihi ya kuzitumia.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Salha Burian, katika banda hilo, Ofisa Masoko wa ASA, Suzan Ludovick, amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuchagua mbegu kulingana na hali ya hewa na mazingira ya maeneo yao.

Amesema ASA inaendelea kuhamasisha matumizi ya mbegu zinazoweza kustahimili changamoto za kimazingira, ikiwemo mahindi aina ya T105, ambayo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, yana uwezo wa kustahimili mazingira yenye ukame na mvua nyingi.

Ameeleza kuwa matumizi ya mbegu zinazolingana na mazingira ya kilimo yanaweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wake, Balozi Dk Burian amezipongeza teknolojia mbalimbali za kilimo zilizooneshwa katika maadhimisho hayo, akisema matumizi ya teknolojia za kisasa na mbegu bora ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo.

Aidha, amewahimiza wananchi, hususan wakulima, kutumia fursa hiyo kujifunza teknolojia mpya za kilimo na kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi bora katika shughuli zao za uzalishaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button