Vijana kunufaika na vifaa vya Sh milioni 458

IRINGA: Vijana wanaosomea taaluma ya misitu nchini wanatarajia kupata ujuzi zaidi unaowawezesha kuajirika, kujiajiri na kuanzisha biashara baada ya Mradi wa Maendeleo ya Misitu, Matumizi ya Ardhi na Mnyororo wa Thamani (FORLAND) kukabidhi basi, mitambo na vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 458 katika Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Mbao (FWITC), Mafinga.

Uwekezaji huo unalenga kupunguza pengo kati ya mafunzo ya darasani na mahitaji halisi ya viwanda, huku ukiimarisha uwezo wa vijana kuchakata mbao na kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa badala ya kutegemea uuzaji wa malighafi pekee.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa katika hafla iliyowakutanisha viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wawakilishi wa Serikali ya Finland, uongozi wa kituo hicho na wataalamu wa FORLAND.

Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa FORLAND, Michael Hawkes, alisema uwekezaji huo unalenga kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa kutumia vifaa vinavyofanana na vile vinavyotumika katika mazingira halisi ya uzalishaji viwandani.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuwapa uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na uchakataji wa mazao ya misitu.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na basi aina ya TATA, mashine ya Wood-Mizer HR200 Resaw, vyombo vya usafiri vya magurudumu matatu aina ya TOYO, kikaushio cha kisasa cha mbao (kiln), mashine za kubana mihimili ya mbao zilizounganishwa na veneer, pamoja na vifaa vya kubebea, kuhamishia na kusogezea malighafi.

Kwa mujibu wa Hawkes, vifaa hivyo vitasaidia kuboresha hatua mbalimbali za mafunzo, kuanzia usafirishaji wa wanafunzi kwenda maeneo ya kujifunzia hadi uchakataji wa mbao na utengenezaji wa bidhaa zenye thamani iliyoongezeka.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa mafanikio ya uwekezaji huo yatategemea namna vifaa hivyo vitakavyotunzwa na kutumiwa kwa ufanisi, akiuomba uongozi wa FWITC kuhakikisha vinafanyiwa matengenezo kwa wakati ili viendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Akizungumzia matokeo ya mradi huo, Mratibu wa FORLAND, Nyachia Roberts, alisema kituo cha Mafinga kimekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo, wakiwamo wale wanaokabiliwa na ushindani wa kupata nafasi katika taasisi nyingine za elimu.

Alisema mfumo wa mafunzo unaosisitiza vitendo umewawezesha wanafunzi kuhitimu wakiwa na uwezo wa kufanya kazi katika mazingira halisi ya viwanda, hali iliyosaidia baadhi yao kupata ajira katika viwanda vya misitu vya Nyanda za Juu Kusini.

“Kwa sasa mahitaji ya wahitimu wetu yamekuwa makubwa kiasi kwamba, kabla hata hawajamaliza mafunzo, viwanda na kampuni mbalimbali hufika hapa kuomba nafasi za kuwachukua vijana hao. Hii ni ishara ya mafanikio makubwa ya mradi,” alisema Roberts.

Alisema ongezeko la mahitaji ya wahitimu linaonyesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya ufundi yanayowaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko badala ya kutegemea maarifa ya kinadharia pekee.

Roberts alieleza kuwa basi lililokabidhiwa litasaidia kupunguza changamoto za usafiri zilizokuwa zikikabili shughuli za mafunzo, ambapo awali kituo kililazimika kutegemea magari machache yaliyokuwepo au kukodi usafiri kwa ajili ya shughuli zake.

Alishukuru Serikali ya Finland kwa ufadhili na ushirikiano wake katika utekelezaji wa mradi huo, huku akiipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia shughuli zake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Misitu katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Seleboni Mushi, alisema vifaa hivyo vitapanua fursa za mafunzo kwa vitendo na kuwawezesha wanafunzi kuelewa kwa karibu teknolojia na taratibu zinazotumika katika sekta ya misitu.

Alisema wizara itaendelea kutoa miongozo na mikakati ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya sekta, sambamba na kusimamia matumizi na utunzaji wa vifaa vilivyokabidhiwa.

Mushi aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Finland umechangia kujenga uwezo wa wadau wa sekta ya misitu na kuimarisha mafunzo yanayohusiana na mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.

Naye mwakilishi wa Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Sanna-Liisa Taivalmaa, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake, akisema Finland inaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza sekta ya misitu kupitia uimarishaji wa mafunzo na kuongeza thamani ya mazao yake.

Alisema ushirikiano huo unalenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaoweza kutumika katika uzalishaji wa bidhaa bora na zenye thamani kubwa, huku ukiimarisha uwezo wa taasisi za mafunzo kuandaa wataalamu wanaohitajika katika soko la ajira.

Alisisitiza umuhimu wa wadau kuendeleza ushirikiano huo ili kuhakikisha uwekezaji katika mafunzo na teknolojia unaleta manufaa kwa vijana, sekta ya misitu na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

FORLAND ni mradi unaolenga kukuza maendeleo endelevu na jumuishi ya sekta ya misitu na minyororo ya thamani ya mazao yake kwa kuimarisha uwezo wa wadau, kuongeza tija na kupanua fursa za kiuchumi kwa wakulima wadogo wa miti na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Kupitia uwekezaji katika mafunzo, teknolojia na uchakataji, mradi huo unalenga kuimarisha matumizi ya miti iliyopandwa, kuongeza ushindani wa bidhaa za misitu na kukuza fursa za ajira na biashara zinazotokana na uzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button