Askari Tanapa, TFS mbaroni mauaji ya wabeba mkaa

KAGERA; Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia askari 13, wakiwemo wa wanyamapori wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na askari mgambo, kwa tuhuma za mauaji ya watu wanne yaliyotokea Kijiji cha Kanyamika, Kata ya Karambi, Tarafa ya Kimwani, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Blasius Chatanda amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 17, 2026 jioni eneo la Kanyamika, kando ya Barabara Kuu ya Muleba- Biharamulo, wakati askari hao walipokuwa doria katika pori la Hifadhi ya Misitu ya Ruiga, Wilaya ya Muleba.
Amesema katika tukio hilo, watu waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa kutumia pikipiki takribani kumi ilidaiwa walikataa kutii amri ya kukamatwa, huku wakitaka kuwanyang’anya askari silaha na kuibua matumizi ya silaha na kusababisha vifo vya watu watatu hapohapo na mmoja hospitalini..
Waliofariki dunia ni Osward Yuster (38), Pius Charles (40), Charles Michael (35) na Edgar Lukangula (44) aliyefariki dunia alfajiri ya jana akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Amewataja watuhumiwa hao ni Mituni Haji (26), Faustin Mboko (25), Kingmar Mewama (40), Fluomena France (28), Erick Muya (25), Yusuph Kweya (26), Emmanuel Zabron (25) na Yusto David (22).
Wengine ni Josiah Mahenge (26), Farouk Mahamudu (24), Baraka Kabulo (28), Regan Bwemelo (24), Alanus Chowe (35) na Andrew Kwiyega (32) anayetajwa kuwa dereva wa TFS.
Amesema polisi imekamata vitu mbalimbali vinavyohusiana na tukio hilo, zikiwemo pikipiki 10, magunia 22 ya mkaa, mapanga matano, kofia ngumu mbili, makoti mawili, silaha tatu aina ya AK-47, maganda matano ya risasi za AK-47.
–



