‘Mabadiliko tabianchi yameongeza ugumu usimamizi rasilimali za maji’

ARUSHA; Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk Toba Nguvila, amesema mabadiliko ya tabianchi yameongeza ugumu na uharaka wa usimamizi wa rasilimali za maji, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha mikakati ya usalama wa maji na ustahimilivu dhidi ya athari za tabianchi.
Dk Nguvila amesema hayo jijini Arusha, alipomwakilisha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, katika ufunguzi wa kongamano la kisayansi la kikanda la siku tatu kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Amesema mabadiliko ya mifumo ya mvua, ukame wa muda mrefu, mafuriko na ongezeko la joto vinahatarisha upatikanaji wa maji, uzalishaji wa kilimo, miundombinu, uzalishaji wa umeme unaotegemea maji pamoja na usalama wa jamii, hivyo kuna haja ya kuimarisha mipango inayozingatia taarifa za tabianchi na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) , Profesa Maulilio Kipanyula, akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema matokeo ya kisayansi yanapaswa kusaidia kufanya maamuzi, kuchochea ubunifu na kutatua changamoto halisi zinazoikabili jamii pamoja na sekta ya viwanda.
Profesa Kipanyula amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kizazi kijacho cha wanasayansi na watafiti, hususan vijana, ambao watakuwa na jukumu la kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu barani Afrika.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Zakia Meghji, ametoa wito wa wanawake kupewa nafasi kubwa katika usimamizi wa rasilimali za maji, tafiti za kisayansi na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha suluhisho la changamoto za maji linazingatia mahitaji ya makundi yote katika jamii.



