Hedwiga atumia sanaa kupinga unyanyapaa wenye usonji

DAR ES SALAAM: Msanii wa sanaa za maonesho na uchoraji, Hedwiga Medard, ametumia kipaji chake cha uchoraji kuelimisha jamii kuhusu changamoto zinazowakabili watu wenye autism ( usonji), magonjwa ya afya ya akili na ulemavu unaoonekana na usioonekana, akihimiza kupunguza unyanyapaa na kujenga jamii inayothamini tofauti zilizopo miongoni mwa watu.

Kupitia maonyesho ya kazi zake yaliyopewa jina la Different, Hedwiga analenga kuongeza uelewa kuhusu Usonji, afya ya akili na umuhimu wa kuwapa watu wenye mahitaji maalum nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.

Hedwiga amesema msukumo wa kuandaa maonesho hayo umetokana na uzoefu wa maisha ya ndugu yake aliyezaliwa akiwa na autism, pamoja na changamoto alizokutana nazo kutokana na ukosefu wa uelewa kutoka kwenye jamii inayomzunguka.

Amesema uzoefu huo umemfundisha umuhimu wa kutumia sanaa kuwasilisha ujumbe ambao wakati mwingine ni vigumu kueleza kwa maneno, hususan namna mitazamo na matendo ya jamii yanavyoweza kuathiri maisha ya watu wenye mahitaji maalumu.

“Natamani jamii itambue athari za maneno na matendo wanayofanyiwa watu wenye changamoto za afya ya akili. Ningependa watu waelewe namna wanavyoweza kuwaathiri wengine, ili kupunguza unyanyapaa na kuwasaidia kuishi katika mazingira bora,” amesema.

Hedwiga amesema alianza kujifunza sanaa za uoni mwaka 2019, akijikita katika uchoraji wa picha kwa kutumia rangi, zikiwamo picha za vitambaa, ukutani na zinazochorwa kwenye karatasi.

Amesema mbali na kutengeneza picha kwa oda za wateja, amekuwa akibuni kazi zake binafsi zinazogusa afya ya akili na maisha ya watu wenye ulemavu, akiamini sanaa inaweza kuwa nyenzo ya kuelimisha jamii na kuchochea mabadiliko ya kijamii.

Akizungumzia gharama za kutengeneza picha, Hedwiga amesema thamani ya kazi ya sanaa haiamuliwi na rangi na vifaa vilivyotumika pekee, bali pia inahusisha muda wa kubuni wazo, kulifanyia kazi na kukamilisha picha yenye ujumbe uliokusudiwa.

Ameongeza kuwa mchakato huo unahusisha pia gharama za kuandaa vitambaa maalumu vya kuchorea vinavyojulikana kama canvas na kutengeneza fremu, ambazo baadhi huziagiza kwa mafundi wa mbao.

Akizungumzia soko la sanaa nchini, Hedwiga amesema bado kuna uelewa mdogo kuhusu baadhi ya kazi za sanaa za uoni, hususan picha za kufikirika ambazo ujumbe wake unaweza kuhitaji maelezo ya ziada ili kueleweka.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka serikali kuongeza juhudi za kuhamasisha na kuendeleza sanaa zinazogusa masuala ya kijamii, ikiwamo afya ya akili, ili ziweze kutumika kuongeza uelewa na kuboresha mazingira ya maisha ya watu wenye mahitaji tofauti.

Katika kuendeleza dhamira ya maonesho ya Different, Hedwiga amesema aliandaa warsha mbili zilizowashirikisha washiriki 20 wenye Autism ( Usonji), waliopata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za sanaa na kushiriki katika utengenezaji wa picha.

Amesema baadhi ya kazi zilizotokana na warsha hizo zimejumuishwa katika maonyesho hayo na zinauzwa, hatua inayolenga kuunganisha ubunifu, ushiriki wa watu wenye Autism na uhamasishaji wa jamii.

Sanaa kurahisisha ujumbe wa afya

Kwa upande wake, Haikaeli Gilliard, mfamasia na msimamizi wa kazi za sanaa zinazowasilisha maudhui ya afya, amesema sanaa inaweza kurahisisha uelewa wa masuala ya afya ambayo wakati mwingine huwa magumu kueleweka yanapowasilishwa kwa njia za kawaida.

Haikaeli amesema amejikita katika kuratibu sanaa kuwasilisha elimu ya afya kwa njia inayoeleweka kwa urahisi, akitolea mfano kazi za Hedwiga zinazogusa Autism na afya ya akili.

Amesema sanaa za maono bado hazijapewa uzito unaostahili, hali inayowafanya wasanii kukabiliwa na changamoto za kupata maeneo ya kuonesha kazi zao na fursa za kuziuza.

Ameongeza kuwa hali hiyo inaweza kuathiri utambuzi wa sanaa za uoni kama shughuli inayoweza kuwa chanzo cha kipato, licha ya muda, ubunifu na gharama zinazotumika katika kutengeneza kazi hizo.

Wito kwa shule na wazazi

Haikaeli amezitaka shule kuimarisha ufundishaji wa sanaa kwa kuwapatia walimu na wanafunzi fursa zinazofaa, akieleza kuwa shughuli za sanaa zinaweza kuwasaidia watoto kujieleza, kukuza ubunifu na kuwasilisha hisia na mawazo yao.

Amesema kuchora kunaweza pia kuwasaidia watoto kujifunza na kuelewa masuala mbalimbali kwa njia zinazowafaa, huku kukiwapa nafasi ya kukuza umakini na ujuzi wa kutumia mikono.

Kwa upande wa wazazi, amewashauri kuwapa watoto nafasi ya kutumia kalamu, karatasi na vifaa vingine vya sanaa nyumbani, badala ya kutegemea vifaa vya kidijitali pekee kwa ajili ya burudani.

Kupitia maonesho ya Different, Hedwiga na Haikaeli wanahimiza jamii kutambua kuwa sanaa si mapambo pekee, bali pia ni nyenzo ya kuelimisha, kujenga uelewa na kufungua fursa kwa watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika maisha ya kila siku.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button