RC Arusha ataka kasi usikilizaji, utatuzi kero za wananchi

ARUSHA; Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amewataka wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa wilaya kuongeza kasi ya kuwafikia wananchi, kusikiliza na kutatua kero zao kwa wakati, akisisitiza kuwa huduma za serikali zinapaswa kuwafikia wananchi bila vikwazo vya usafiri.
Makalla amesema viongozi hao wanapaswa kutumia vitendea kazi walivyopatiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ikiwemo kutembelea maeneo mbalimbali, kufuatilia changamoto za wananchi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Ametoa agizo hilo jijini Arusha wakati akikabidhi magari manne kati ya matano yaliyonunuliwa kwa Sh bilioni 1.2 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa serikali katika wilaya za Mkoa wa Arusha.
Magari hayo yalikabidhiwa kwa mkuu wa wilaya ya Arusha na makatibu tawala wa Wilaya za Longido, Ngorongoro na Arumeru.
Amesema upatikanaji wa magari hayo ni sehemu ya dhamira ya Rais Samia kuhakikisha viongozi na watumishi wa Serikali wanakuwa na vitendea kazi vinavyowawezesha kuwafikia wananchi na kuwahudumia kwa wakati.



